Pasina nadharia ya kimapinduzi hapawezi kuwa na harakati za kimapinduzi
Mawazo ya kimapinduzi huwa nguvu za kimapinduzi yanapowafikia umma
Marx, Engels na Lenin
Yaliyomo:
1. Utangulizi: kuelewa uhuru na haki za binadamu
1.1. Umuhimu wa ufafanuzi wa uhuru na haki za binadamu
1.2. Msimamo nitakaouzingatia katika mjadala huu
1.1. Je, ni nini maana ya haki za binadamu?
1.3. Uhusiano wa uhuru na na haki za binadamu
1.4. Maendeleo, uhuru na haki za binadamu
2. Historia ya haki za binadamu
2.1. Utangulizi: mifumo ya uzalishaji
2.2. Msamiati wa siasa-uchumi
2.2.1. Kuzaana na kuzalisha
2.2.2. Vitu vya kufanyia kazi, vitu vya kufanyiwa kazi na nguvukazi
2.2.3. Njia ya uzalishaji, nyenzo za uzalishaji na mfumo wa uzalishaji
3. Uhuru na haki za binadamu katika mfumo wa umajumuihalisi
4. Gurudumu la historia daima huzunguka mbele
5. Mfumo wa umajumuiuliyokomaa
6. Mabadiliko kutoka mfumo mmoja hadi mwingine
7. Mfumo wa Utumwa
8. Mfumo wa Ukabaila
9. Mfumo wa ubepari
9.1. Historia ya mfumo wa ubepari
9. 2. Demokrasi ya kibepari
9.3. Harakati za kitabaka
9.4. Makinzano ya ubepari na chimbuko cha ubeberu
10. Ubeberu
10.1. Ubeberu
10.2. Ukolonimkongwe
11.2. Ukolonimamboleo
1. Utangulizi: kuelewa uhuru na haki za binadamu
1.1. Umuhimu wa ufafanuzi wa uhuru na haki za binadamu
Ukitaka kuutibu ugonjwa wowote ule kikamilifu sharti kwanza uuelewe kabisa, ufahamu kiini chake barabara. Ni daktari mbaya sana ambaye ataanza kumtibu mgonjwa kabla hajafanya utafiti wa kitaalamu wa kufahamu ugonjwa wake. Tunapambana dhidi ya udikteta na ubeberu. Tunapigania ukombozi wa kijamii na kitaifa, uhuru, demokrasi na haki za binadamu katika nchi yetu. Je, tuna maana gani tukisema hivi?
Ni muhimu tuyaelewe kwa marefu na mapana mapambano yetu. Tufahamu kiini chake na madhumuni yake. Ni muhimu lengo la kimsingi la mapambano yetu lieleweke vema kwetu, kwa umma, na hata kwa adui. Tunaposema tunapigania uhuru na haki za binadamu tuna maana gani hasa? Ni nini tunadai? Tunataka mambo yawe vipi ndiyo turidhike, maadamu haturidhiki hata kidogo na maisha katika kipindi hiki cha historia ya nchi yetu?
Lengo la insha hii ni kutoa mchango wangu wa kujibu maswali kama haya na kuchochea mjadala huu kwa mwelekeo wa kimapinduzi. Maadamu, swala la haki za binadamu linajadiliwa kila siku nchini na viongozi wa kidini, mawakili, wabunge, waandishi wa habari, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wa Kenya kwa ujumla, sitasita hata mimi kutoa maoni yangu. Na katika kufanya hivyo, nitatekeleza haki yangu ya binadamu ya kutumia nadharia ya kimapinduzi, mtazamo wa Kimarx kuhusu haki za binadamu. Kwani ni nadharia ya Kimarx ambayo inatoa mwelekeo wa kweli wa kufafanua na kupigania utekelezaji wa haki za binadamu. Maana shabaha ya mapinduzi ya kisoshalisti ni utekelezaji wa haki za binadamu.
Aidha, nadharia ya Kimarx itatusaidia tu ikiwa tutaisoma na kuielewa barabara na pia kuitumia kuelewa na kutafsiri vilivyo hali halisi ya nchi yetu, historia yake, siasa zake, uchumi wake na utamaduni wake. Hii ni kwa sababu Umarx ni mawazo ya kimapinduzi na mawazo kimapinduzi huwa nguvu za kumapinduzi wakati yanapowafikia umma. Hii ndiyo kwa sababu katika insha hii tunazingatia historia ya nchi yetu tunapojadili swala nyeti la uhuru na haki za binadamu.
1.2. Msimamo nitakaouzingatia katika mjadala huu
Nitachukua msimamo wa kitabaka na kutumia njia ya uyakinifu wa kihistoria, kama kawaida yangu, katika mjadala huu kuhusu uhuru na haki za binadamu. Nikizingatia hali halisi ya taifa letu, nitazungumza kutoka kwa msimamo wa tabaka la wafanyikazi na wakulima makabwela, kutoka kwa macho ya wachochole, kutoka kwa umma unaotamani na kupambania ukombozi. Nitatoa maoni yangu kama mzalendo, kama mwanamapinduzi na kama mtu ambaye hivi sasa ninashiriki katika harakati za ukombozi.
Nia ya insha hii ni kudhihirisha kwamba maana ya uhuru na haki za binadamu ya mabepari, mabeberu, vibaraka wa mabeberu kwa upande mmoja, ni tofauti kabisa na ile ya wafanyikazi, wakulima-makabwela, umma na wanamapinduzi kwa upande mwingine. Aidha, tumeona na tutaendelea kuona kuwa maana ya haki za binadamu kwa mabepari na mabeberu kwa upande mmoja ni tofauti na ile ya usoshalisti kwa upande mwingine.
Hata hivyo, Ingawa maana ya uhuru na haki za binadamu inaeleweka tofauti kwa matabaka tofauti na yanayopingana, hii haina maana kuwa hakuna maana halisi ya uhuru na haki za binadamu. Chambilecho Fredrick Engels, ingawa ukweli na uongo unategemea hali halisi na adili ya mtu binafsi au tabaka halisi finyu, hata hivyo ukweli hauwezi kuwa uongo na uongo hauwezi kuwa ukweli.
1.3. Je, ni nini maana ya haki za binadamu?
Haki zako za binadamu ni yale mambo yote ambayo ni yako kwa mujibu wa kuwa binadamu. Ulizaliwa na haki zako za binadamu kwa sababu tu wewe ni binadamu. Kwa mfano, maisha ni haki yako ya binadamu, tena ya kimsingi. Hii ina maana kwamba kwa sababu umezaliwa, upo, uhai ni haki yako wala huhitaji kuomba ruhusa kutoka kwa mtu yoyote yule ili uishi. Isitoshe, hakuna mtu yoyote yule aliye na haki juu ya uhai wako, hakuna mwenye haki halali ya kukuzuia kuishi, ya kukuua. Na endapo mtu akakuua kwa sababu yoyote ile, basi atakuwa amekunyang’anya haki yako ya kimsingi, uhai.
Haki yako ya binadamu ni kile kilicho chako kwa kuwa wewe ni mtu, ni binadamu. Mathalani, tunaposema haki za uraia, tuna maana kuwa ni zile haki zote ambazo lazima uwe nazo kwa mujibu wa kuwa raia wa nchi yako, kama kuishi kwa amani na usalama na tena pasina kunyanyaswa na serikali ama mtu yoyote yule, huku ukiwa na njia halali ya kujipatia riziki na kujiendeleza kwa kila hali. Kumnyima mtu haki yake ni kumnyanyasa, ni kumgandamiza, ni kumvua utu wake. Watu waliyo chini ya himaya ya ubeberu wananyanyaswa, hawako huru kwa kuwa wananyimwa haki yao kama binadamu ya kujitawala na kujiamulia sudi yao wenyewe kama taifa.
Ndiyo kwa maana tunasisitiza kwamba kuwa chini ya ukoloni ama ukolonimamboleo ni kuporwa haki za binadamu, na kwa hivyo kupambana dhidi ya ukoloni na ukolonimamboleo ni haki ya binadamu. Kwa maneno mengine, mapambano ya ukombozi wa kijamii na kitaifa, mapambano dhidi ya ubepari na ubeberu, ni mapambano ya haki za binadamu vilevile.
Tunaposema elimu na matibabu ni haki ya kila raia, tuna maana kuwa, kwa sababu tu umezaliwa katika nchi hii, kwa kuwa wewe ni mwananchi na mtu unayeishi hapa, unastahili kupata elimu na matibabu. Elimu na matibabu si kitu ambacho utasaidiwa nacho na serikali, bali ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa wewe kama mwananchi na kama mtu unapata elimu na matibabu, unapata haki yako ya elimu na matibabu.
Na kwa kuwa elimu na matibabu ni haki yako basi si sahihi kuuziwa ama kupewa. Wala elimu na matibabu si msaada kutoka kwa serikali, ni haki yako. Hivyo, kununua elimu na matibabu kutoka kwa serikali kama ilivyo nchini hivi sasa, ni makosa na ni kinyume cha haki za binadamu. Ubinafsishaji wa taasisi za huduma za elimu na afya ni uvunjaji wa haki za binadamu.
Huwezi kuuziwa au kupewa kile kilicho chako, huwezi kutunikiwa haki zako za binadamu kama zawadi. Kwani, tunakariri, haki zako za binadamu ni yale mambo unayostahili kuwa nayo kwa sababu tu wewe ni binadamu. Haki zako za binadamu ni ubinadamu wako.
Katika sura ya nne ya Katiba ya Kenya, kuna orodha ndefu ya haki za binadamu. Ilichukua miaka mingi ya mapambano kulazimisha orodha hiyo kuwa sehemu ya katiba ya nchi yetu. Hata hivyo, kama tutakaposoma katika sehemu nyingine ya insha hii, ni muhali kutekeleza kikamilifu na ipasavyo orodha hii ya haki za binadamu kwani Kenya ni ya mfumo wa kibepari. Na mfumo wa kibepari ni mfumo wa kuvunja haki za binadamu kwani ni mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Nao unyonyaji ni uvunjaji wa haki za binadamu.
1.4. Uhusiano wa uhuru na na haki za binadamu
Hadi sasa tumeeleza kuwa haki za binadamu ni yale yote binadamu anastahili kuwa nayo kwa mujibu wa kuwa binadamu, na ambayo akinyang’anywa atakuwa amenyanyaswa. Kwa mfano, demokrasi, uhuru wa kutembea, kujumuika, kusafiri, kusema, amani, ajira, maji masafi, nyumba, njia halali ya kujipatia riziki, afya, uhai, zote ni haki za binadamu.
Kwa kweli orodha ya haki za binadamu ni ndefu kuliko ile ya Katiba ya Kenya, Umoja wa Kimataifa na ile ya Shirikisho la Afrika. Maana orodha ya haki za binadamu ni kubwa na haina kikomo. Kikomo chake ni kufa kwa binadamu.
Na hapa tunafika kwa swali, ni kweli haki za binadamu ni mambo yale yote binadamu anastahili kuwa nayo ama kutendewa kwa mujibu wa kuwa binadamu. Lakini, je, binadamu anapata mambo yote anayostahili kupata kama binadamu? Binadamu anatekeleza haki zake zote za binadamu alizozaliwa nazo? Binadamu wote wanaweza kuishi kwa afya, furaha, amani na bila usumbufu hadi wakazeeka na kufa? Inawezekana kutekeleza haki za binadamu kila mara kwa maneno na kwa vitendo? Chakula bora, nguo bora, nyumba bora, maji masafi, elimu, matibabu, usalama wa kijamii, na kadhalika, zote ni haki za binadamu, lakini je kila mwananchi au kila binadamu anatekeleza haki hizi? Je, kila binadamu ulimwenguni anatekeleza haki zake zote za binadamu?
Haya maswali ambayo majibu yake ni rahisi, wazi na bayana kwa kila mwananchi na binadamu mwenye akili timamu, ni ya kimsingi katika kufafanua na kuhakiki mjadala wetu kuhusu haki za binadamu kwa kina. Kwa sababu majibu ya maswali haya ni kuwa ijapokuwa kila mtu ana haki ya kuishi, kwa mfano, si kila binadamu anayezaliwa anatekeleza haki yake hii ya kimsingi. Wengine wanakufa wakiwa bado matumboni mwa mama zao, wengine wanakufa baada ya kuzaliwa tu, wengine kwa maradhi ama kwa njaa, ajali ama kwa vita, na kadhalika. Wengi wanaishi maisha magumu ya ufukara, nyanyaso na dhiki za kila aina. Wakati huohuo kuna binadamu wengine ambao wanafurahia maisha zaidi na kuishi muda mrefu na kwa amani na usalama zaidi kuwaliko wengine na hivyo wanafurahia haki za binadamu zaidi katika maisha kuwaliko binadamu wengine.
Kwa ufupi, tunasema hapa kuwa kuna tofauti kati ya kuwa na haki za binadamu na na kuteleza haki hizo katika hali halisi ya maisha. Tunakariri: orodha ya haki za binadamu ni kubwa sana, lakini orodha ya utekelezaji wa haki za binadamu ni ndogo mno ulimwenguni.
Mantiki hii inatusongeza hatua nyingine mbele zaidi katika ufafanuzi wetu wa mada hii. Haki za binadamu zina historia kama kitu chochote kingine katika maisha. Haki za binadamu hukua na kuongezeka kutekelezeka na kuzidi kuonekana katika hali halisi ya maisha kadiri jamii ya binadamu inavyokua na kuendelea. Hivyo, kuna uhusiano mkubwa sana kati ya haki za binadamu na uhuru. Bila ya kufahamu maana ya kisayansi ya uhuru hatuwezi kuelewa, kufahamu na kutafsiri ipasavyo maswala kuhusu haki za binadamu.
1.5. Maendeleo, uhuru na haki za binadamu
Kabla hatujaendelea zaidi, inafaa katika hatua hii kusisitiza kuwa katika mjadala huu wote, sisi hatuzungumzii uhuru wa kidhahania, uhuru wa kudhania na kufikiria tu ambao hauwezi kushikika wala kuonekana katika hali halisi ya maisha. Yaani hatuzungumzii uhuru unaozungumzwa na wanaozingatia falsafa ya kibwanyenye kuhusu uhuru.
Mara kwa mara, kwa mfano, utawasikia wadhalimu wakisema ati Kenya ni nchi huru, ati tunajitawala wenyewe sisi weusi, na tuliufukuza ukoloni kabisa tangu mwaka wa 1963. Utawasikia wakiropoka na kupayuka usiku na mchana pasina aibu wala haya ati hapa kwetu hatuna ubaguzi, ati sote tuko sawa, maskini na matajiri. Ati maskini yuko huru kuingia, kula, kulala na kustarehe kwa hoteli ya aina yoyote ile kama tajiri, mwajiri ama mtalii! Na kwa kweli uhuru wa aina hii unaonekana katika katiba ya kitaifa ya Kenya ya sasa.
Lakini, je, ni kweli kuwa katika hali halisi ya maisha nchini, maskini, mfanyikazi ama mkulima kabwela, anaweza kuingia, kula, kulala na kustarehe katika hoteli yoyote ile kama tajiri, mwajiri ama mtalii? Jibu ni wazi na bayana, kuwa haya yote si kweli wala hayawezekani, kwani mapato ya maskini, mfanyikazi au mkulima kabwela, hayawezi kumwezesha kuingia, kula, kunywa, kulala na kustarehe katika mahoteli makubwa ya kifahari yaliyojaa Nairobi, Mombasa, Malindi, Taita, Narok, Kwale, Kilifi, Lamu, Naivasha na sehemu nyingi nchini. Tunaelewa sote kuwa anasa na starehe na maisha mazuri nchini ni kwa ajili ya matajiri wa kienyeji na watalii kutoka Ulaya na penginepo ulimwenguni.
Mfano mwingine: Tunaelezwa na viongozi wa nchi yetu, na hata na katiba ya Kenya, ati kila Mkenya ana haki ya kutembea pahali popote anapotaka pasina kikwazo chochote kile. Hata hivyo, hii si kweli kwani kutembea kunahitaji pesa. Hivyo, tajiri ana uwezo wa kutumia gari, ndege na meli, na kwa hivyo ana uhuru wa kusafiri na kutembea zaidi kuliko kabwela ama mchochole.
Pamoja na hayo, ni muhimu kukumbuka kuwa kabla ya magari, ndege, meli na vyombo vingine vya usafiri kugunduliwa, uhuru wa binadamu wa kutembea ulikuwa haba mno, mtu hangeweza kusafiri mbali kutoka pahali alipozaliwa. Wala haingeyumkinika kusafiri kutoka Dawida, kwa mfano, hadi Marekani, Uchina, Ulaya na nchi zingine za mbali. Kuongezeka kwa elimu, ujuzi, ufundi, sayansi na tekinolojia kila wakati kumekuwa kukimwongezea binadamu uwezo wa kutengeneza vyombo vya kusafiria. Na kuongezeka kwa wingi na ubora wa vyombo vya kusafiria kumekuwa kukimwongezea binadamu uhuru wa kusafiri. Bila shaka binadamu wa leo ana uhuru zaidi wa kusafiri kuliko binadamu wa awali kwani hivi leo binadamu anasafiri hadi mwezini, Mars, na sayari zingine.
Aidha, kukua na kuongezeka kwa sayansi na tekinolojia ya madawa na matibabu, kilimo na uzalishaji chakula, utengenezaji nguo bora na bora zaidi, kuwa na vifaa bora zaidi, haya yote yaliongeza uhuru wa binadamu wa kuishi na kufurahia maisha kikamilifu zaidi kuliko hapo awali. Kwani hapo awali maradhi, ukosefu wa chakula bora na cha kutosha, baridi, miali ya jua na maadui wengine wa afya ya binadamu, yalihakikisha kuwa uhuru wa binadamu wa kuishi, na kuishi muda mrefu iwezekanavyo na kwa furaha na amani, ulikuwa kidogo mno. Haya tutayafafanua kwa kirefu punde si punde.
Kwa sasa tunataka kusisitiza kuwa kuna uhusiano wa kipembuzi kati ya uhuru na maendeleo. Maana maendeleo ni kuongezeka kwa ujuzi na uwezo wa binadamu wa kuyaelewa na kuyatumia maumbile kwa ajili ya kutosheleza mahitaji yake. Maendeleo ni uboreshaji wa hali, maisha. Na kila hali na maisha yanavyozidi kuboreka ndiko vilevile uhuru wa binadamu unavyokua na utekelezaji wa haki za binadamu unavyoongezeka.
Uhuru sharti utosheleze mahitaji ya binadamu, na kwa sababu hii tunaweza kusema pia kuwa uhuru ni kuongezeka kwa uwezo na ujuzi wa binadamu wa kuzielewa sheria zinazotawala maumbile (sayansi) na kuzitumia kuzalisha (tekinolojia) yale yote ya kuboresha maisha yake. Kwa ufupi, uhuru ni hali ya utekelezaji wa haki zake za binadamu. Kwa hivyo, kila kunapokuwa na maendeleo, uhuru unaongezeka na kila uhuru unapoongezeka uwezo wa binadamu wa kutekeleza haki zake za binadamu nao unaongezeka vilevile.
Tunakariri, uhuru si kitu kilichosimama bali ni kitu chenye historia, kinachoenda na wakati kwani uhuru unakua na kubadilika jinsi jamii yenyewe inavyokua na kubadilika. Maendeleo hudhihirisha hali ya kwenda mbele, kukua na kubadilika kwa ubora na ni kinyume cha hali ya kurudi nyuma, kusimama, kuharibika na kutobadilika. Chambilecho Julius Kambarage Nyerere, uhuru na maendeleo ni kama yai na kuku, bila uhuru hapawezi kuwa na maendeleo, na bila maendeleo hapawezi kuwa na uhuru.
Kwa maneno mengine, kuna uhusiano wa kipembuzi kati ya uhuru na maendeleo. Haya yote tutayafafanua hapa mbele kwa kutumia mifano halisi katika maisha ya kila siku na historia ya binadamu na ya nchi yetu. Tunalotaka kulisisitiza kwa kiwango hiki ni kuwa kadiri kunapokuwa na maendeleo, ndivyo uhuru wa binadamu unavyoongezeka na vilevile ndivyo uwezo wa kutekeleza haki za binadamu unavyoongezeka.
Haki za binadamu, kwa hivyo, zina historia: zimekuwa zikikua, yaani zimekuwa zikizidi kutekelezeka, kadiri jamii yenyewe imekuwa ikikua na kuendelea. Kila uhuru unapoongezeka ndipo uwezo wa binadamu wa kutekeleza haki zake za binadamu unavyoongezeka. Kwa sababu hii, ili kulijadili kikamilifu swala la haki za binadamu, itatupasa tujadiliane kuhusu historia ya binadamu kwa ujumla, na vilevile historia ya nchi yetu.
2. Historia ya haki za binadamu
2.1. Utangulizi: mifumo ya uzalishaji
Historia ya binadamu imepitia viwango vifuatavyo katika kipindi kimoja ama kingine: mfumo wa umajumui, mfumo wa utumwa, mfumo wa ukabaila, mfumo wa ubepari na sasa binadamu wanaelekea katika mfumo mpya na wa hali ya juu zaidi, mfumo wa ukomunisti.
Tutajaribu kuona jinsi jinsi uhuru na haki za binadamu hukua, kuongezeka na kutatanika kutoka mfumo wa hali ya chini hadi ule wa hali ya juu. Tutakapomaliza kufanya hivyo, tutakuwa tumepata picha ya maana ya uhuru na haki za binadamu, tutakuwa tumefahamu kwa hakika na pasina tawashishi maana ya mapambano yetu na lengo la hatimaye la mapambano ya uhuru, demokrasi na haki za binadamu yanayopamba moto katika nchi yetu. Tutafahamu harakati za ukombozi kufungamana na nadharia ya kimapinduzi, kutoka kwa mtazamo wa tabaka la wavujajasho, tabaka la makabwela, tabaka la umma, tabaka la wengi.
2.2. Msamiati wa siasa-uchumi
Kabla hatujaanza kujadili kuhusu mifumo ya uzalishaji tuliyoitaja hapa juu, ni muhimu kufahamu, ijapokuwa kijuujuu tu, maana ya kisayansi ya maneno ya kiistilahi ambayo tutayatumia katika mijadala yetu ya siasa uchumi.
2.2.1. Kuzaana na kuzalisha
Kwanza kabisa msingi wa maisha ni kuzaana na kuzalisha. Kuzaana ni hali ya binadamu kuongezeka, kupata watoto. Kuzalisha ni shughuli yoyote ya binadamu ambayo inamwezesha binadamu kujipatia mahitaji yake kutoka kwa maumbile au kutengeneza vitu. Kutafuta riziki: chakula, nguo, malazi, na kadhalika ni uzalishaji. Shughuli za kiuchumi, kilimo na viwanda vilevile ni uzalishaji mali.
Tunaposema kuzaana na kuzalisha ndiyo msingi wa maisha tuna maana gani? Tuna maana kuwa bila ya kuzaliwa hatuwezi kufikaria kuhusu jambo lolote lile kwa kuwa hatupo na kwa hivyo hatuna haki za binadamu kwa kuwa bado hatujakuwa binadamu. Na endapo tukazaliwa, halafu tukafa, tukose kuishi, vilevile hatuwezi kuwa na haki za binadamu maana hatukukaa, tulikufa.
Ili tuishi, tukaae duniani hai, tuwe na haki za binadamu, tunahitaji mambo ya kimsingi: chakula, nguo na malazi. Na ili tuwe na mahitaji haya ya kimsingi kwa maisha duniani, lazima tuyatafute kwa njia moja ama nyingine, lazima tufanye kazi, tushughulike. Na, tunakariri, huko kufanya kazi ya kutafuta kutosheleza mahitaji yetu ya kila siku ni uzalishaji. Ni muhimu kukumbuka falsafa hii kwani kiini cha mawazo yote ya binadamu ni binadamu mwenyewe, akiwa hai, na kuwa hai kunatokana na uzalishaji. Kwa hivyo, chimbuko cha mambo mengine yote ya binadamu, mkiwemo mawazo, hatimaye ni uzalishaji, na hali kadhalika kuzalisha ndiko kufanya utamaduni, ndiko kufanya historia. Haya ndiyo yanafyotufanya tuseme wanyama hawafanyi utamaduni, hawana historia, wanaishi tu katika historia, kwa sababu hawazalishi kwa maksuudi kama binadamu wanavyofanya.
2.2.2. Vitu vya kufanyia kazi, vitu vya kufanyiwa kazi na nguvukazi
Sasa ili kuzalisha kitu chochote kile, kiwe kidogo ama kikubwa kiasi gani, tunahitaji mambo matatu muhimu, vitu vya kufanyia kazi (kwa mfano vifaa), vitu vya kufanyiwa kazi (kwa mfano ardhi au malighafi) na nguvukazi (binadamu na uwezo wake wa kufanya kazi). Vitu vya kufanyia kazi ni vyombo vyovyote vile kutoka jembe, panga, hadi mashini za hali ya juu zinazotumika katika viwanda vya siku hizi, njia za usafirishaji na mawasiliano, na mazao yote ya sayansi na tekinolojia ya uzalishaji. Na vitu vinavyofanyiwa kazi ili vizalishe vingine ni ardhi, malighafi kama madini, udongo, saruji, mbao, mazao ya kilimo, na kadhalika, ikitegemea ni kitu kinachozalishwa. Nguvukazi ni kazi ya binadamu mwenyewe na akili zake na mwili wake ambaye anaifanya kazi kwa kutumia vifaa na malighafi ama ardhi ili kuzalisha mahitaji muhimu ya binadamu.
Na kati ya haya matatu, nguvukazi ndiyo msingi wa uzalishaji, ndiyo muhimu zaidi. Hata hivyo, lazima ieleweke kwamba mojawapo wa haya matatu ikikosekana hapawezi kuwepo na uzalishaji wa chochote kile. Kwa mfano, kukiwa na unga na maji (malighafi) na moto, mwiko na sufuria (vitu vya kufanyia kazi) halafu kukosekane mpishi (nguvukazi) hatuwezi kupata ugali. Na mpishi akipatikana pamoja na moto na mwiko na sufuria halafu kukosekane unga na maji hatuwezi kula ugali. Aidha, kukiwa na unga na maji pamoja na mpishi lakini kukosekane sufuria na mwiko kwa vyovote vile ugali haupikiki. Hivyo, kwa kila kitu kinachozalishwa, sharti kuwepo na vitu vya kufanyia kazi, vitu vya kufanyiwa kazi na nguvukazi. Tunasema kuwa nguvukazi ndiyo muhimu zaidi katika uzalishaji kwa sababu binadamu (nguvukazi) ndiye anayeamua kuhusu uzalishaji, yeye ndiye anayefanya mambo haya mawili mengine, kuunda vitu vya kunyia kazi na kutumia vitu vya kufanyiwa kazi, kushiriki katika uzalishaji.
2.2.3. Njia ya uzalishaji, nyenzo za uzalishaji na mfumo wa uzalishaji
Vitu vya kufanyia kazi vikijumlishwa na vitu vya kufanyiwa kazi vinaitwa njia za uzalishaji mali. Kwa mfano, tunaweza kusema kwamba njia kuu ya uzalishaji ya watu wengi wa Kenya ambao ni wakulima makabwela ni ardhi na vifaa duni vya jembe na panga, na wakati mwingine jembe la kukokotwa na ng’ombe. Pia trekta inaendelea kutumika siku hizi ijapokuwa kwa uchache. Njia ya uzalishaji mali ni pamoja na ardhi, misitu, maji, madini, malighafi, vifaa vya uzalishaji, pahali pa kuzalishia, njia za usafirishaji na mawasiliano na kadhalika. Basi njia za uzalishaji mali zikijumlishwa pamoja na nguvukazi zinakuwa nyenzo za uzalishaji. Na nyenzo za uzalishaji ndiyo msingi wa uzalishaji, ndizo zinazolisukuma gurudumu la historia mbele, ndizo zinazobadilisha sura ya dunia na kuipamba kwa alama ya kazi za binadamu – utamaduni. Nyenzo za uzalishaji ndizo msingi wa maendeleo na mabadiliko yoyote katika historia.
Tusonge mbele. Katika shughuli za uzalishaji, watu huingiliana, hufanya kazi pamoja, huuziana, hubadilishana mazao na bidhaa, huwasiliana, yaani huhusiana kwa njia moja ama nyingine kwa kuwa kitendo cha uzalishaji ni kitendo cha kijamii wala siyo cha kibinafsi. Uchumi huhusu mahusiano ya watu katika jamii. Sasa haya mahusiano ya watu katika uzalishaji ndiyo yanayoitwa mahusiano ya uzalishaji ama mahusiano ya kijamii-kiuchumi. Nayo mahusiano ya uzalishaji yakijumlishwa na nyenzo za uzalishaji yanafanya mfumo wa uzalishaji. Kwa hivyo, mfumo wa uzalishaji ambao tunaweza kuuita mfumo wa kijamii-kiuchumi, unahusu jinsi watu (jamii) wanavyozalisha, jinsi wanavyohusiana na jinsi wanavyotumia ama kugawanya kile ambacho wanakizalisha.
Mifumo ya uzalishaji mitano inayojulikana katika historia hadi sasa ni mfumo wa umajumui, mfumo wa utumwa, mfumo wa ukabaila, mfumo wa ubepari na mfumo wa ukomunisti (ambao unaendelea kukua).
3. Uhuru na haki za binadamu katika mfumo wa umajumuihalisi
Mfumo wa umajumuihalisi, ndiyo mfumo wa kwanza unaojulikana katika historia ya binadamu. Katika mfumo huu, pengo kati ya binadamu na masokwemtu, ambao ndiyo babu na bibi zetu binadamu katika historia ya maumbile, lilikuwa ndogo sana. Kwani uhuru wa binadamu ulikuwa mdogo mno, uwezo wake wa kuzielewa sheria za maumbile, kuzitawala na kuzitumia kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake, ulikuwa haba mno. Ndiyo kwa maana mfumo wa umajumuihalisi unaitwa pia mfumo wa umajumui wa kishenzi.
Katika kiwango hiki binadamu alijipatia chakula kutokana na uchumaji, usasi na uvuvi wa kishenzi ambao ulitumia silaha duni kama mawe na vijiti, na vilevile ulitegemea misuli zaidi kuliko akili ama maarifa. Ikawa hata kuwinda mnyama mmoja kulihitaji kushirikiana kwa idadi kubwa ya watu ambao pengine wangemzingira mnyama huyo na kumfukuza hadi anapoanguka kwa kuchoka. Vilevile, binadamu alijipatia chakula kwa kusaka na kuambua matunda na mizizi ya porini, karibu sawa na wanyama wengine.
Hivyo, katika hali hii, kazi ya kutafuta chakula ilichukuwa muda mrefu, ilikuwa na mazao madogo na ilihitaji nguvu nyingi na kumshirikisha kila mtu katika jamii, wazee kwa vijana, watoto kwa watu wazima, wanaume kwa wanawake. Na kwa vile kila mtu alihitajika katika uzalishaji huu wa asili, kile kilichowindwa au kuzalishwa kiligawanywa kwa insafu, kwa usawa, kufungamana na mahitaji ya kila mtu.
Maskani ya watu wa umajumuihalisi yalikuwa ya kishenzi, walikuwa wakiishi mapangoni, chini ya au juu ya miti au katika maskani ovyo yaliyotengenezwa kwa kukusanya majani ama matawi pamoja. Wala katika kiwango hiki binadamu hakuwa ameanza kufuga wanyama ama mimea. Hivyo, hapakuwa na kilimo katika mfumo wa umajumuihalisi.
Kwa sababu hii, tunaona kuwa uhuru wa binadamu wa umajumuihalisi ulikuwa haba sana, kutokana na uwezo wake haba wa kuzielewa, kuzitawala na kuzitumia sheria za maumbile kuzalisha mahitaji yake. Binadamu bado hakuwa amejikomboa kwa kiasi kikubwa kutoka kwa maumbile, bali alitegemea maumbile karibu kwa kila hali, aliishi chini ya himaya ya maumbile, alitegemea huruma za maumbile kwa ajili ya uhai wake. Na kwa bahati mbaya, maumbile hayana huruma kwa kuwa hayana hisia, na kwa sababu hii kulingana na binadamu wa leo, maisha ya binadamu katika mfumo wa umajumuihalisi yalikuwa magumu, ya njaa, ukosefu, ushenzi, dhiki tilatila na mafupi.
Ni muhimu hapa kukumbuka kuwa hata katika kipindi hiki cha historia yake, binadamu alikuwa na haki zote za binadamu tulizo nazo leo, maana alikuwa binadamu. Bali haki hizi hazingeweza kutekelezeka, isipokuwa kidogo sana, maadamu uhuru wake ulikuwa haba mno. Alikuwa na haki ya kuishi, tena kuishi kwa muda mrefu iwezekanavyo, na kwa amani, furaha na maendeleo. Alikuwa na haki ya shibe, kula chakula bora, kuwa na nguo nzuri za kufaa, kuwa na nyumba bora, kupata elimu na matibabu bora, na kadhalika. Haki hizi zote na zingine zilikuwa zake kama binadamu, bali hangeweza kuzipata, kuzifaidi, kuzifurahia na kuzitekeleza katika hali halisi ya maisha ya mfumo wa umajumuihalisi.
Ijapokuwa alikuwa na haki ya kutumia ardhi na maliasili yoyote jinsi alivyopenda, hangeliweza kutekeleza haki hii isipokuwa kidogo mno kwa kuwa hakuwa na ujuzi wa kutosha wala vifaa vya kutosha vya kufanya hivyo. Ukosefu huohuo wa ujuzi na maarifa ya kutosha na vifaa vya kutosha ulikuwa na maana kuwa hangeliweza kupata chakula bora na cha kutosha jinsi alivyohitaji ama kutaka. Vilevile, hangeliweza kuwa na nguo na maskani bora ya kufaa. Haya yote na mengine ambayo hakuwa na uwezo wa kuyapata yana maana kuwa hakuwa huru kuishi muda mrefu, na kwa hivyo haki yake ya binadamu ya kuishi muda mrefu iwezekanavyo, na kwa amani na salama, ilikuwa inatekelezeka kwa kiasi kidogo sana.
Maradhi na ukosefu wa matibabu na madawa muhimu yana maana kuwa hakuwa na haki kubwa ya kufurahia afya nzuri na wengi walikuwa wanakosa haki yao ya kuishi kabisa, kwani walizaliwa wakiwa tayari wamekufa, ama walipozaliwa tu walikufa ama kutokana na maradhi, njaa ama ajali zilizokuwa nyingi sana na ambazo hazikuwa na kinga. Ukosefu wa maskani bora na nguo una maana kuwa haki yao ya kuishi muda mrefu na kufurahia maisha ilizidi kuwa hata ndogo zaidi.
Na wakati kulipokuwa na ukame, mafuriko ama ungonjwa hatari wa kuambukizana, idadi kubwa ya watu ilikuwa ikiangamia pamoja wakati mmoja na kuporwa haki yao ya maisha na maumbile kama enzi za Nuhu katika Bibilia. Ndiyo kwa maana, katika kiwango hiki ambapo binadamu walikuwa wakidhibitiwa na maumbile, idadi ya watu ilikuwa ndogo mno na ilikuwa ikiongezeka polepole sana.
Idadi ya watu ilikuwa ndogo. Watu walikuwa wakiishi kwa makundi madogomadogo ya jamaa, mbari na koo. Tena tunaweza kuongeza kuwa, ijapokuwa kila mtu alikuwa na haki ya kusafiri pahali alipotaka, lakini ukweli ni kwamba hawakuweza kutekeleza haki yao hii kikamilifu, kwani kulingana na hali halisi ya historia yao, hawangeweza kusafiri mbali kutoka pahali walipozaliwa. Muda wao mwingi kila siku, siku nenda rudi, ulitumika katika kujitafutia riziki ambayo, kama tulivyoona, haikuwa rahisi kupatikana. Ukosefu wa vifaa na silaha bora haungewaruhusu kujasiri nyika na misitu yenye wanyama hatari. Katika hali ambapo hapakuwa na vyombo vya kusafiria majini kama ngalawa, mitumbwi, mashua ama meli, mto mdogo ulionekana kama bahari, sembuse bahari yenyewe!
Kwa muhtasari, katika mfumo wa umajumuihalisi, binadamu alitekeleza haki zake kwa kiasi kidogo mno, kwa kiasi ambacho tunaweza kusema kuwa hakuwa na uwezo wa kutekeleza haki zake kutokana na uhaba wa uhuru wake kutoka kwa maumbile. Lakini, je, kwa sababu uhuru na haki za binadamu huhusu uhusiano kati ya binadamu na maumbile na pia kati ya binadamu na binadamu, mahusiano ya watu katika mfumo wa umajumui yalikuwaje? Yalisababisha uhuru kati ya mtu na mtu ama yalizidisha nyanyaso?
Tumeona kuwa uhaba wa uhuru, kutoelewa sheria za maumbile na kuzitumia kusababisha maendeleo, kumpatia binadamu mahitaji yake, kumpunguzia njaa, tabu, dhiki, umaskini na ujinga, kulileta hali ya watu kuwa pamoja ili kushirikiana kujihahami na kuzalisha mahitaji yao. Kwa mfano, kila mtu mzima na mwenye afya katika jamaa, koo ama mbari, alishiriki katika kutafuta chakula. Na kwa kuwa kila mtu alifanya kazi ya kutafuta chakula basi kilichopatikana kiligawanywa kwa usawa na kulingana na mahitaji ya kila mtu. Haikuwa rahisi kukipata wala chakula hakikuwa kinapatikana mara kwa mara, lakini wakati kilipopatikana kila mtu alitekeleza uhuru na haki ya kula sehemu yake sawa na mtu mwingine yoyote yule kufungamana na mahitaji yake na wingi wa chakula chenyewe. Maadamu hapakuwa na ziada, hali ya mtu mmoja kujinyakulia na kujilimbikizia chakula kingi kuliko wengine au kuzidi mahitaji yake haikuweko. Hakuna aliyeweza kuwanyima wenzake haki zao juu ya chakula walichokitafuta kwa kushirikiana wote pamoja.
Hali ya uchoyo, ulafi, ubinafsi na unyonyaji wa mtu kwa mtu haingewezekana kwani pia idadi ndogo ya watu iliwafanya waishi kwa makundi ya kijamaa, kikoo na kimbari, watu waliyokuwa na uhusiano wa kidamu ambapo ilikuwa vigumu na muhali kunyanyasana wenyewe kwa wenyewe.
Na muhimu hata zaidi, maadamu kila mtu alifanya kazi muhimu ya kutafuta riziki, ilifuata kuwa watu wote walikuwa sawa, wanaume kwa wanawake, wazee kwa vijana, watoto kwa watu wazima, wote walikuwa sawa. Hapakuwa na kundi lolote la watu ambao walinyimwa haki zao za binadamu na binadamu wenzao. Katika kiwango hiki wanawake waliheshimiwa sana hasa kwa kuwa watu walihitajika mno katika jamii hii, kwani wanawake ndiyo waliyohusika moja kwa moja katika kuzaa na kuongeza idadi ya watu. Wala hapakuwa na fikra hata kidogo kuwa wanaume ni bora kuliko wanawake katika mfumo wa umajumuihalisi.
Vilevile, kwa kuwa idadi ya watu ilikuwa ndogo na mali ya ziada na ya binafsi haikuwa imejitokeza, watu wote walikuwa na uhuru sawa wa kutembea, kusafiri na kufurahia ardhi na maliasili jinsi walivyotaka. Ardhi na maliasili yalikuwa milki ya kila mtu wala siyo mali ya mtu ama watu binafsi. Kila mtu alikuwa huru kufanya jinsi anavyotaka bora tu asitumie haki hii kupinga adili za mfumo huu ambazo ziliundwa kuhifadhi amani, umoja, ushirikiano, utangamano, ujamaa na mahusiano ya kidamu na kikoo, na kuweka masilahi ya jamaa na jamii mbele ya masilahi ya binafsi. Adili hii ilisisitiza kuheshimiwa kwa haki za kila mtu katika jamii pasina ubaguzi wowote ule. Kwa muhtasari, katika jamii ya mfumo wa umajumuihalisi kulikuwa na usawa katika utekelezaji wa haki za binadamu.
4. Gurudumu la historia daima huzunguka mbele
Hapa ni muhimu tupumue kidogo ili tupate nafasi ya kusisitiza kuwa gurudumu la historia daima huzunguka mbele. Historia ya binadamu kila mara i mbioni, inasonga mbele, inakwenda na wakati, mara polepole mara kwa kasi, mwendo wa kikonakona, wa kiupogoupogo, lakini mwendo ni wa mbele tu kila mara. Kumbuka tumeeleza hapo awali kwamba kile kinachosababisha historia msingi wake ni kukua kwa nyenzo za uzalishaji, kuongezeka kwa ujuzi na uwezo wa binadamu wa kutengeneza vifaa na kuvitumia kufanya maumbile (ardhi, misitu, madini, malighafi, na kadhalika) kumzalishia mahitaji yake kwa wingi na kwa ubora zaidi kila siku, huko ndiko kuzalisha utamaduni, ndiko kufanya historia, ndiko kupamba dunia kwa ustaarabu.
Kwani kutengeneza vifaa, vyombo, na kuzalisha chochote kile, ndiko kunakopamba na kubadilisha sura ya dunia na kutangaza uhai wa binadamu duniani, ndiko kunakozidisha pengo kati ya binadamu na wanyama, ndiko tunakokuita utamaduni. Na kuzalisha utamaduni ndiko kufanya historia, ndiko kuboresha maisha, kufanya maendeleo, kustaarabika. Na kadiri binadamu anavyoendelea kitamaduni, ndivyo uhuru wake kutoka kwa maumbile unavyozidi kuongezeka, ndivyo uwezo wake wa kuzitekeleza haki zake za kiasili za binadamu unavyozidi.
Kwa hivyo, kutoka mwanzo binadamu amekuwa akipiga hatua mbele kimaendeleo, kitamaduni, kihistoria. Hata kama ni polepole vipi, alikuwa akiendelea mbele tu, na wala hakuna pahali popote duniani ambapo binadamu amekuwapo halafu akawa amesimama, akawa amekwama siku zote, akawa hazalishi utamaduni au hafanyi historia.
Mabeberu wanapodai kuwa ati sisi watu weusi hatukuwa tunafanya historia, ati hatukuwa tunazalisha utamaduni kabla ya ukoloni mkongwe kutuvamia, huo ni upuuzi, ujinga na uhange usiyo na msingi wowote ule wa ukweli wa historia. Ndiyo, ni kweli, jinsi utamaduni wa watu unavyotofautiana, jinsi mazingira yao yanavyotofautiana, ndivyo vilevile mwendo wao wa kufanya historia unavyotofautiana. Maumbile yenyewe ndiyo yamesababisha binadamu wengine kuwa mbele kihistoria kuliko binadamu wengine, wala si kwa sababu binadamu wengine wana akili zaidi kuwaliko binadamu wa rangi zingine. Binadamu wote ni sawa kwa mujibu wa kuwa binadamu pasina kujali rangi, kabila, tabaka, jinsia wala pahali walipozaliwa na wanapoishi.
Hoja tunayotaka kuwasilisha katika kiwango hiki cha mjadala wetu ni kwamba kila mara katika historia kuna jamii ya binadamu ambao walikuwa mbele kitamaduni na kimaendeleo kuliko jamii zingine za binadamu. Hii ina maana kuwa jamii za binadamu wengine zimekuwa huru zaidi kuliko zingine, na hii, aidha, inamaanisha kuwa jamii zingine zimekuwa na uwezo zaidi wa kutekeleza haki zao za binadamu kuliko jamii zingine, ingawa wote ni binadamu wakiwa na haki sawa za binadamu. Hii pia ndiyo sababu ya kimsingi ambayo iliwawezesha binadamu wengine kuwavamia binadamu wenzao, kuwatawala, kuwanyonya, kuwanyanyasa, kuwanyang’anya haki zao za binadamu. Lakini haya tutayajadili kwa kirefu hapo mbele.
6. Mfumo wa umajumuiuliyokomaa
Mfumo wa umajumuiuliyokomaa*, ni kiwango cha juu zaidi na cha mwisho cha mfumo wa umajumui. Katika kiwango hiki mfumo wa umajumui umekua na kukomaa na kufikia kilele chake ambapo sharti uzae mfumo mwingine mpya na wa hali ya juu zaidi. Tunaweza kukisia kuwa ilichukuwa maelfu au hata mamilioni ya miaka kwa binadamu kutoka kwa mfumo wa umajumuihalisi hadi kufikia mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Wakati wakoloni walipovamia nchi yetu, makabila mengi katika nchi yetu yalikuwa katika viwango mbalimbali vya mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Wajaluo, Wakikiyu, Wadawida, Wamijikenda, Wameru, Wakisii, Wakalenjin, Wamaasai, Wasomali, Waborana, Wakamba, Waluhya na kadhalika, wote walikuwa katika kiwango kimoja ama kingine cha mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Hata mawazo ya ujamaa yanayoelezwa kuwa msingi wa usoshalisti wa Mwafrika na watu mashuhuri kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Tom Mboya na wengineo, kwa kweli ni mawazo ambayo yanahusu kipindi cha mfumo wa umajumuiuliyokomaa katika historia ya binadamu. Na mara kwa mara watu wanapozungumza kuhusu utamaduni wa Kenya ama wa Kiafrika, huwa wanazungumzia utamaduni katika kipindi hiki cha historia, mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Aidha, ni muhimu kusisitiza kuwa, siyo sisi Waafrika, Wakenya ama watu weusi peke yake ambao tulipitia kipindi hiki cha historia ninachokiita mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Historia haina ubaguzi wa rangi kwa mkabala huu. Historia ya binadamu wote duniani ilipitia katika viwango mbalimbali vya mfumo wa umajumui.
Kulingana na mfumo wa umajumuihalisi, mfumo wa umajumuiuliyokomaa, ulikuwa maelfu ya miaka mbele kimaendeleo. Katika kiwango hiki, miaka mingi kabla ya kuwasili kwa ukoloni, watu wa Kenya walikuwa wamepiga hatua nyingi sana mbele kitamaduni, na hivyo walikuwa huru zaidi. Tayari walikuwa wakitekeleza haki zao za binadamu kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko hapo awali.
Kwani tayari walikuwa wakitumia vifaa mbalimbali, mkiwemo vya shaba na chuma. Hii ina maana kuwa walikuwa wameendelea sana kisayansi na kitekinolojia. Kuweza kuutambua udongo wenye chuma au shaba na ukauchuja hata ukapata chuma ama shaba nyekundu kunahitaji aina fulani ya elimu ya kemia na fizikia. Hali kadhalika kutengeneza matanuri na hewa ya oksijini ya kupandisha halijoto za juu sana za kuweza kuyeyusha vyuma, halafu ukatumia hivyo vyuma kutengeneza majembe, visu, panga, mishale, mikuki na vifaa na vyombo mbalimbali hakika kunahitaji aina fulani ya sayansi na tekinolojia ambayo bila shaka mababu zetu walikuwa nayo kabla ya uvamizi wa ukoloni.
Sasa kuwa na sayansi na tekinolojia hii kuliwawezesha kufua vyuma, shaba, shaba nyekundu na madini mbalimbali na vilevile kuliwawezesha kuongeza uwezo wao wa kuyanyonya na kuyatumia maumbile kwa ajili ya kutosheleza mahitaji yao. Kwa mfano, kwa kutumia hii sayansi na tekinolojia waliendeleza kilimo chao kwa kutengeneza majembe, mapanga na vifaa vingine. Tayari walikuwa wameweza kufuga aina nyingi ya mimea na mifugo kwa ajili ya mahitaji yao ya chakula, nguo, uwindaji, ulinzi, dawa, na kadhalika. Katika mfumo wa umajumuihalisi, hapakuwa na ufugaji wowote ule, uwe wa mimea uwe wa mifugo, binadamu alitegemea bahati kutoka kwa maumbile kama wanyama pori.
Kufuga mbwa, kwa mfano, kuliwawezesha babu zetu kurahisisha kazi ya kuwinda na vilevile kuongeza mawindo kwa ajili ya mahitaji yao. Wakati huohuo mbwa alifanya kazi nyingine muhimu ya kuwalinda kutoka kwa maadui wao. Kufuga kuku, bata, mbuzi, kondoo, ng’ombe, ngamia na kadhalika kuna maana kuwa hawa wanyama wangeweza kuzaana kwa wingi na ukubwa zaidi na vilevile kuwa karibu zaidi kwa ajili ya nyama, maziwa, mayai, samadi, ngozi, na kadhalika. Pia kufuga mimea kama migomba, mihogo, viazi, nduma, mtama, njugu na aina mbalimbali za mboga, nafaka na mimea ya mizizi, na kuzilima mashambani badala ya kuzitafuta porini zinapomea vururumtende, kulisaidia kupatikana kwa haya yote kwa urahisi, kwa wingi, kwa uhakika na kwa ubora zaidi.
Kwa ufupi, kilimo kiliongeza chakula na hivyo utekezalaji wa haki ya binadamu ya kuishi kwa muda mrefu na kwa amani na furaha zaidi. Kwani upungufu wa hatari ya njaa, kuongezeka kwa chakula bora, kuliwawezesha kufurahia afya bora zaidi kuliko awali. Kutokana na kukua kwa kilimo, haki ya shibe na kula chakula bora kilichowawezesha kuwa na afya bora zaidi, ilizidi kudhihirika na kutekelezeka katika maisha yao. Tena walikuwa huru zaidi kutoka kwa maumbile, kwani badala ya kutegemea maumbile tu kwa mahitaji yao ya chakula, walipiga hatua mbele kuzielewa sheria za maumbile na kuanza kuzitumia kufuga wanyama, ndege na mimea – kilimo. Kwa hivyo, njaa na maisha ya bahati na sibu na kuishi kwa huruma za maumbile yakawa mbali zaidi na wao kulingana na hapo awali. Pengo kati ya binadamu na wanyama likazidi kupanuka.
Vilevile, hali ya kuongezeka kwa chakula, shibe na afya bora katika jamii, kulisababisha kuongezeka kwa idadi ya watu, na kuongezeka kwa idadi ya watu kuliongeza uhuru wao zaidi. Kwani watu wakiwa wengi wanaweza kuzalisha zaidi, kuvumbua mengi zaidi, kusanii utamaduni zaidi na kujihami vyema zaidi. Hata wahenga wetu walisema, ‘penye wengi pana mengi’. Na uchumi huhusu mahusiano ya watu katika jamii.
Kuwepo kwa vifaa bora zaidi kuliko hapo awali, kuliwasaidia binadamu kujenga maskani bora zaidi. Kweli, wakoloni walipofika hawakutukuta tukiishi mapangoni au chini ya miti kama wanavyodai. Tulikuwa tukiishi kwa nyumba. Nyumba zilizojengwa kwa miti, udongo na kuezekwa kwa nyasi au udongo, kutegemea utamaduni wa jamii halisi. Tena zilijengwa kwa taratibu, mpangilio na mantiki yake, yaani zilikuwa na usanifu wa kujenga wa hali ya juu kwa wakati wake. Nyumba hizi ziliweza kuwalinda binadamu kutokana baridi, jua kali, mvua, wanyama hatari na kumwezesha kuishi katika mazingira ya amani, starehe, salama na furaha zaidi. Hivyo binadamu akaongeza uhuru wa kutekeleza haki yake ya kuwa na maskani bora na ya kufaa na kuwepo kwa maskani mazuri kukaongeza utekelezaji wa haki yake ya kuishi muda mrefu na kwa raha zaidi.
Kufuga wanyama na mimea na kuwa na vifaa kuliwasaidia watu wetu kutengeneza nguo bora zaidi kuliko hapo awali na hivyo kuongeza uwezo wao wa kutekeleza haki ya binadamu ya kuvaa nguo bora na maridadi za kumsetiri kutoka kwa aibu na madhara yanayotokana na kutokuwa na nguo.
Elimu yao ya miti pia iliwawezesha kufanya mambo mengi. Walitumia aina fulani ya za miti kujitengezea dawa mbalimbali na hivyo kuongeza uhuru wao wa kujikinga na maradhi na kuzidisha utekelezaji wa haki yao kama binadamu ya kupata matibabu, kuwa na afya bora na hivyo kuishi muda mrefu na vyema zaidi.
Ukoloni ulitukuta tukiwa tuna ujuzi wa kutengeneza vyombo vingi vya aina tofautitofauti kutoka kwa miti, mawe, vyuma, nyasi, udongo na kadhaliaka. Kwa mfano, kutoka kwa miti watu wetu walikuwa wakitengeneza vinu, teo, nyuta, mikuki, mishale, nyungo, vikapu, vidasi, miko, vijiko, mikoba, sahani, viti, bakuli na vyombo mbalimbali.
Kwa muhtasari, tunaweza kusema kwa sahihi kabisa na pasina shaka yoyote kuwa tulikuwa tumepiga hatua kubwa sana mbele katika kuzalisha utamaduni halisi wa kutosheleza mahitaji ya kimsingi ya chakula, nguo, malazi, vifaa na vyombo tilatila. Yaani katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, uhuru wetu ulikuwa si haba kulingana na pahali tulipokuwa tumetoka kama binadamu, na kila siku tuliendelea kuongeza uhuru wetu na haki zetu za binadamu zilizidi kudhihirika na kutekelezeka zaidi na zaidi.
Sasa, watu wakiwa na uwezo, ujuzi na vifaa wataweza kuzalisha, siyo tu mahitaji yao ya kimsingi, bali ziada. Aidha, watakuwa na muda na uwezo zaidi wa kutengeneza vitu vya kujiburudisha na kujistarehesha, kama ala za muziki, ngoma, na kadhalika. Na watu wakishiba na wakiwa na afya bora watazalisha sanaa ya kuweza kujiburudisha kwa tamasha mbalimbali kama ngoma, muziki, tamthilia na michezo. Kwa ufupi watapata fursa ya kuzalisha utamaduni wa fikra. Wakati wa mfumo wa umajumuihalisi, kutokana na uhaba wa uhuru, iliwapasa watu kila mara kuwa katika harakati za kujitafutia riziki tu na kujihami. Kutokuwa na vifaa kulikuwa na maana kuwa hapakuwa na uwezo wa kutengeneza vyombo vya sanaa mbalimbali kama ngoma na ala za muziki wala wakati wa kushiriki katika sanaa. Hivyo, ijapokuwa binadamu katika mfumo wa umajumuihalisi alikuwa na haki ya kujiburudisha, kuzalisha na kufurahia sanaa, hakuwa na uwezo wa kutekeleza kwa kiwango kikubwa haki yake hii ya kuzaliwa.
Bali katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, kukua kwa sayansi na tekinologia, kuliwawezesha kuzalisha chakula cha kutosha na hata zaidi, na kupata nafasi ya kupumzika, kufikiria, kusanii na kujiburudisha kwa muziki, ngoma, na starehe tilatila. Inaeleweka ulimwenguni kuwa Mwafrika alikuwa mbele sana katika uwanja huu wa utamaduni wa akili wa kutekeleza haki yake ya kujiendeleza kimawazo, kustarehe na kujiburudisha.
Maendeleo yalimpatia binadamu uhuru zaidi hata akapata nafasi ya kuketi kuwaza na kuwazua kuhusu maisha, falsafa ikachipuka, ikakua na kunoga na ikajidhihirisha katika sanaa kama fasihi-simulizi (ngano, methali, vitendawili, tenzi za kusimulia historia ya koo, mbari ama watu mashuhuri, na kadhalika; uchoraji, uchongaji, ufinyajnzi, na kadhalika). Aidha, dini, mila na desturi zikakua. Yaani kadiri nyenzo za uzalishaji zilivyokua ndivyo utamaduni halisi na utamaduni wa akili, wa kuwasilisha hisia za binadamu kwa twasira, ulivyozidi kukua, kuongezeka kwa upeo, kupevuka na kutatanika.
Sina budi kuongeza kuwa katika kipindi hiki cha historia, uhuru wa kutembea na kusafiri uliongezeka zaidi, binadamu alisafiri mbali zaidi akaona mengi zaidi na upeo wake kuhusu dunia ukawa mkubwa zaidi kuliko hapo awali. Ufugaji wa mbwa, punda, ngamia na utengenezaji wa silaha za kujihami, yote yalimwezesha binadamu kujasiri nyika na misitu zaidi na zaidi kila siku. Kuwepo kwa vifaa kulimwezesha kutengeneza vyombo vya kusafiria majini kama mitumbwi na ngalawa, vilevile kutengeneza maulalo na daraja ndogondogo, yote yalipunguza vikwazo vya kuzuia uhuru wa kusafiri na kutembea. Na wakati wa kiangazi binadamu aliweza hata kutumia maji kunywesha mimea, unyunyizaji, na hivyo kila siku akazidi kuongeza uwezo wake wa kutoishi chini ya huruma za maumbile na kutegemea maumbile kama wanyama pori.
Katika mfumo wa umajumuihalisi, watu waliishi kwa makundi madogomadogo ya jamaa, mbari na koo, lakini katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, ingawa mahusiano ya mbari na koo bado yalikuwa muhimu sana, tayari watu walifika kiwango cha kujiona, kujihisi na kujitambua kama kabila. Hili liliwezeshwa na kuongezeka kwa idadi ya watu na hivyo maeneo yao ya kijiografia na kiuchumi. Kwa mfano, kabla ya kuja kwa ukoloni Kenya, kulikuweko na makabila ya Wakamba, Wakikuyu, Wajaluo, Waluhyia, Wakisii, Wadawida, Wasomali, Waborana na kadhalika. Isitoshe, sasa Wadawida, kwa mfano, walijua kuna makabila mengine kama Wagiriama, Wakamba, Wachaga, Wasambaa, Wapare, Wamasai na kadhalika.
Kuongezeka kwa uhuru wao wa kusafiri kuliwawezesha Wadawida kukutana, kujuana, kuingiliana, kufanya biashara na kuathiriana na watu wa makabila jirani kwa njia moja ama nyingine. Pia uhuru wao uliwawezesha kutalii mazingira yao na kupanua mipaka yao ya kijiografia kadiri walivyohitaji kufanya hivyo, hasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu. Na maendeleo haya yakaleta migogoro na migongano ya kimbari na kikabila kama tutakavyoona punde si punde.
Pamoja na haya yote, mfumo wa umajumuiuliyokomaa uliendelea kuwa mfumo usiyo wa kitabaka. Kabla ya kuwasili kwa wakoloni nchini, haya makabila yetu tuliyoyataja hapa juu hayakuwa na tabaka la watawala na watawalwa, wanyonyaji na wanyonywaji, matajiri na maskini. Njia kuu ya uzalishaji, ardhi, ilimilikiwa na jamii yote kwa ujumla na wala hapakuwa na mali ya binafsi, iliyotumiwa kutajirisha watu wachache kwa kazi na jasho la wengi wengine. Kila mtu mwenye afya na uwezo alikuwa anafanya kazi ya kujizalishia mahitaji yake na ya jamaa yake.
Na maadamu njia kuu ya uzalishaji, ardhi, ilikuwa mikononi mwa jamaa na koo, na kwa vile mahusiano ya watu hubadilika pole pole zaidi kuliko nyenzo za uzalishaji, katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, bado kulikuwako na mabaki ya adili za mfumo wa umajumuihalisi. Adili za mfumo wa umajumuiuliyokomaa bado zilikuwa zikisisitiza kuhusu thamani ya umoja, usawa, ushirikiano, ukarimu, huruma, umuhimu wa mahusiano ya kidamu, na kadhalika. Zilikuwa zinapinga ubinafsi, ulafi, ukatili, uzembe na unyonyaji wa mtu kwa mtu.
Hata hivyo, tulisema hapo awali kuwa mfumo wa umajumuiuliyokomaa ulikuwa na mimba pevu ya mfumo mpya na wa kiwango cha juu zaidi. Kukua kwa nyenzo za uzalishaji katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, kulizidisha mali katika jamii hiyo. Hivyo, kukatokea ziada, ziada ya chakula, mifugo na mazao mengine. Watu wakaanza kujilimbikizia mali, na kukawa na watu wengine ambao walikuwa na chakula na mifugo mingi zaidi kuwaliko wengine. Ingawa bado ziada hii haikuwa mali ya binafsi, yaani haikutumika kujiongeza kwa kunyonya jasho la wengine, bali tayari wenye mali zaidi kuliko wengine walianza kuwa na sauti zaidi, walianza kuathiri jamii zaidi, walianza kutekeleza haki za kidemokrasi zaidi kuliko wengine katika jamii. Kukawa na hali ya watu wengine kuwa na uwezo wa kutumia mali yao kuwanyonya na kuwanyanyasa wengine.
Chinua Achebe ameyasimulia haya kwa ustadi katika vitabu vyake mashuhuri, Shujaa Okonkwo na Mshale wa Mungu. Jamii za Ki-Igbo anazozizungumzia Achebe katika ruwaya hizi ni mfano mzuri wa jamii ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Kukua kwa nyenzo za uzalishaji, vilevile kulileta aina mpya ya ugamvi wa kazi katika jamaa na katika jamii ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa kwa ujumla. Katika jamaa, ugamvi wa kazi za nyumbani ulihakikisha kuwa wanaume nyumbani walifanya kazi chache na ndogo zaidi kuliko wanawake. Hali hii ilileta mahusiano ya kuwanyanyasa wanawake. Taasubi ya kiume ikakua na kukomaa ambayo, kwa mfano, ilifundisha ati kazi za nyumbani kama kupika, usafi, kulisha watoto, kusafisha vyombo, na kadhalika ati ni kazi za wanawake. Wanaume wakajihesabu kuwa bora zaidi kuliko wanawake. Kukawa na tabia ya kuoa wanawake wengi ili kupata watu wa kuwatumikia nyumbani, shambani na kuwazalia watoto wa kuwatumikia. Kukawa na mila ya mahari ambayo ilitumika kuwauza wasichana kwa wanaume kwa mifugo na mali zingine na hivyo kuzidi kuwadunisha wanawake. Kwa ufupi, adili za wanawake kunyanyaswa na wanaume zikakua katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Ndipo ikawa kuwa maendeleo yaliyokuwa yanaletwa na kukua kwa nyenzo za uzalishaji, yaliongeza uhuru kutoka kwa maumbile, lakini wakati huohuo yakaleta unyanyasaji wa mtu kwa mtu ambapo wanawake walinyanyaswa na wanaume, nao watoto na vijana wakagandamizwa na wazee katika jamii. (Katika insha nyingine, tutaeleza kwa marefu na mapana, jinsi wanawake walivyoanza kugandamizwa na wanaume, na umuhimu wa mapambano ya ukombozi wa wanawake kwa kuwa hatuwezi kamwe kuwa huru kama jamii wakati kuna ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia).
Katika jamii, tunaona kuwa ugamvi wa kazi ulileta watu wa ujuzi, usanii na ufundi, kama wahunzi, wachongaji, maseremala, wafinyanzi, washonaji na waganga wa kila aina. Hawa wakaanza kutumia ujuzi, ufundi na usanii wao kufanya kazi kidogo zaidi – lakini kazi ya utaalamu na yenye thamani – kuliko wengine, wakaanza kuwa na hadhi na haki zaidi katika jamii kuliko wengine kwa kutumia vipawa vyao. Kwa mfano, kwa kazi ndogo, lakini ya ujuzi, ya kufua chuma na kutengeneza kifaa cha jembe, ilikupasa umpe mhunzi gunia moja la maharagwe; kwa kukung’oa jino ilikupasa umpe mganga gunia moja la mtama; ili mchongaji kukutengenezea mchi na kinu, labda ulihitajika kutoa gunia mbili za mihogo, viazi na kunde, na kadhalika. Ukienda kupigiwa ramli na mganga ilikubidi uchukue kuku nyeupe na mbuzi mweusi, na kadhalika. Hii ina maana kuwa watu wenye ujuzi, ufundi na maarifa muhimu katika uchumi wa jamii, walianza kuwa na mali kuliko wengine, kwa kufanya kazi kidogo lakini ya utaalamu mkubwa wakajinunulia haki ya kufanyiwa kazi, kulishwa, kutajirishwa na kuheshimiwa kuliko wengine. Nao viongozi wa kidini, waliyoshikilia mila, desturi na tamaduni za jamii, wakaanza kutumia fursa walizokuwa nazo kujilimbikizia mali zaidi kuliko wengine. Haya pia yanajitokeza vizuri sana katika ruwaya ya Achebe, Mshale wa Mungu, kupitia kwa mhusika wake mkuu, Ezeulu.
Hali hii, iliyoletwa na ugamvi wa kazi uliyowezekana kwa kukuwepo kwa ziada, ilileta adili mpya ya uchoyo na ubinafsi ambapo wenye ujuzi wowote ule, uwe ni wa uhunzi, uganga, uchongaji, ufinyanzi, utabiri na kadhalika walianza kuuhodhi na kuufanyia ukiritimba. Hivyo, ujuzi ukawa ni siri ya jamaa, mbari ama koo fulani tu, wala usiruhusiwe kutoka na kuenea kwa watu wengine katika jamii. Elimu ikaanza kutumiwa kuwanyonya na kuwanyanyasa wengine. Kwani ikiwa kila mmoja angelikuwa na ujuzi wa kufua vyuma na kutengeneza vifaa na vyombo vingine muhimu, mathalani, mhunzi hangekuwa na watu wa kuwanyonya, kuwanyanyasa na wa kumtajirisha. Adili hii ya ubinafsi na uroho, ya jamaa chache maalumu kuficha elimu, ujuzi, maarifa na usanii bila shaka ilichelewesha kusambaa (na inaendelea kuchelewesha) kwa maendeleo ya sayansi na tekinolojia katika jamii, haikosi ilikuwa (na inaendelea kuwa) sehemu ya kikwazo cha kukua kwa maendeleo, kwa uhuru.
Aidha, tayari tumesema kwamba, kukua kwa nyenzo za uzalishaji, kulikowezesha kuwepo kwa ziada, kulisaidia katika kuongeza idadi ya watu katika jamii. Kuongezeka kwa idadi ya watu kulikuwa na maana kwamba watu walihitaji lishe na ardhi kubwa zaidi kuliko hapo awali. Hivyo migogoro katika jamii na baina ya jamii za mfumo wa umajumuiuliyokomaa iliyohusu matumizi ya maliasili kama ardhi, machungaji na maji ikawa sasa inajitokeza kwa wingi zaidi kuliko hapo awali. Hili pia limesimuliwa vizuri sana na waandishi mashuhuri wa riwaya, Chinua Achebe (Shujaa Okonkwo na Mshale wa Mungu) na Elechi Amadi (The Concubine) wanaomulika jamii za Ki-Igbo (Nigeria) ambazo zilikuwa katika kiwango hiki cha mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Asateaste kukaanza kuwa kwamba mwenye nguvu za mali, silaha, misuli na watoto, anakuwa na uwezo zaidi wa kuwanyang’anya wengine haki zao za kumiliki ardhi. Pia kukaanza kuwa na vita vya kimbari na kikabila vya kupigania ardhi iliyoendelea kuwa njia kuu ya uzalishaji katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Kupanua mipaka ya ardhi kwa ajili ya kulima ama kulisha mifugo ikawa kiini cha vita vya wenyewe kwa wenyewe, na vita baina ya kabila moja na lingine. Kabila lililokuwa na watu wengi zaidi, na silaha nyingi na bora zaidi, na uwezo zaidi wa kivita na kisilaha likawa na uwezo wa kulivamia kabila lingine, kulinyang’anya ardhi, mifugo, chakula, hata watu. Wenye uhuru zaidi wakawa wenye haki zaidi juu ya wengine, wakatumia uhuru wao kunyanyasa wengine, kuwazuia kutekeleza haki zao za binadamu.
Kwa muhtasari, ikawa kwamba, kukua kwa nyenzo za uzalishaji mali kukaanza kutatizwa na mahusiano ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Kwa maneno mengine, mahusiano ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa, ambayo bado hayakuwa ya kitabaka, yakaanza kuzuia kukua na kuongezeka kwa uzalishaji mali. Mahusiano ya umajumui yakawa yanaleta vikwazo kwa kuongezeka kwa uhuru wa jamii. Kukawa kuna makinzano kati ya nyenzo za uzalishaji na mahusiano ya uzalishaji. Katika historia, suluhisho la makinzano haya ni kuzaliwa kwa mfumo mpya wa uzalishaji wa hali ya juu zaidi. Wajaluo, Wakamba, Wamijikenda, Wakalenji, Wamasai, Wakikuyu, Wadawida, na kadhalika walikuwa wamefikia sehemu moja ama nyingine ya kiwango hiki wakati ukoloni ulipowasili katika nchi yetu.
Kuwasili kwa ukoloni kukaua mtoto wa mfumo mpya tumboni lilipevuka kabla hajazaliwa na kumpachika mama wa mfumo wa umajumuiuliyokomaa mtoto mgeni wa bandia wa mfumo wa ubepari wa kikoloni, mahusiano ya uzalishaji ya unyonyaji wa mtu kwa mtu.
Tutakariri kusisitiza kuwa, kabla ya kuwasili kwa ukoloni, tulikuwa tunapiga hatua mbele kila siku za kuongeza uhuru na utekelezaji wa haki za binadamu. Wakenya hatukuwa tumesimama. Tulikuwa tunaendelea kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, kisayansi, kitekinolojia na kwa kila hali. Uhuru wetu ulikuwa ukiongezeka, na hivyo uwezo wetu wa kutekeleza haki zetu za binadamu ulikuwa ukiongezeka. Aidha, maendeleo pia yalikuwa yakileta makinzano katika jamii kuhusu kuelekea katika kugawanya jamaa kitabaka na kuleta mahusiano ya unyonyaji na udhalimu wa mtu kwa mtu. Na wakati ukoloni ulipotuvamia, tulikuwa katika kiwango cha juu na cha mwisho cha mfumo wa umajumui, tulikuwa kwa mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Tayari tulikuwa tunaanza kuingia kwa mfumo wa kitabaka. Ukoloni ukaparaganya mkondo wa maendeleo yetu ya kihistoria.
6. Mabadiliko kutoka mfumo mmoja hadi mwingine
Ni muhimu kusisitiza kuwa kabla ya uvamizi wa ukoloni, kuna baadhi ya Wakenya, Waswahili, wanaoishi katika ufuo wa bahari na pwani ya Kenya, Mombasa, Lamu, Siu, Pate, Malindi, na kadhalika, ambao walikuwa katika mfumo wa utumwa-ukabaila, yaani tayari walikuwa wamepitia mfumo wa utumwa na walikuwa katika kiwango cha chini cha mfumo wa ukabaila ambacho bado kilikuwa na masalia ya mahusiano ya mfumo wa utumwa. Kwa sababu hii, ufahamu kuhusu mfumo wa utumwa na ule wa ukabaila, kutatusaidia kufafanua vizuri hoja tunayowasilisha katika insha hii.
Na ili kuelewa mfumo wa utumwa, ni muhimu kukumbuka yafuatayo: kwamba, kihistoria, mfumo wa utumwa ulizaliwa na mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Hata hivyo, ikiwa ilimchukua binadamu mamia ya maelfu ya miaka kutoka kwa mfumo wa umajumuihalisi hadi mfumo wa utumwa, ilimchukua binadamu miaka elfu chache kufikia mfumo wa ukabaila kutoka kwa mfumo wa utumwa, ikitegemea hali halisi katika sehemu mbalimbali za ulomwengu. Kwani kadiri binadamu alivyoendelea, ndivyo nyenzo za uzalishaji zilivyokua kwa kasi zaidi, na ndivyo mahusiano ya kijamiikiuchumi yalivyobadilika kwa haraka zaidi.
Pia, tulisema kuwa nyenzo za uzalishaji hukua na kubadilika haraka zaidi kulingana na mahusiano ya uzalishaji. Tukaona kuwa hata baada ya maelfu na maelfu ya miaka, bado mahusiano ya mfumo wa umajumuihalisi (na itikadi zake) yaliendelea kusalia na kuathiri watu katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Hali kadhalika, kwa kuwa historia ya binadamu hutii sheria halisi za maendeleo ya kijamii, ambazo ziko nje ya uwezo wa binadamu, kubadilika kwa mfumo mmoja hadi mwingine si kitendo cha kidharura (isipokuwa kunapofanyika mapinduzi ama uvamizi wa mataifa mengine yaliyoko katika mfumo wa hali ya juu zaidi kama vile ukoloni ulivyovamia Kenya), si kitendo cha kufumba na kufumbua wala si kitendo cha mwendo wa msitari uliyonyoka. Katika historia ya binadamu kabla ya ubepari, mabadiliko yalifanyika polepole, taratibu, na asteaste. Ndiyo kwa sababu tumeona kuwa dalili za mfumo wa kitabaka, utumwa, zilianza kujitokeza na kuonekana katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa na watu wakaishi nazo kwa miaka na miaka katika huohuo mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Tukizingatia mantiki hii, tutaelewa kuwa mwanzoni mwa mfumo wa utumwa, bado kulikuwako na mahusiano ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa wakati mmoja sawia na mahusiano mapya ya mfumo wa utumwa. Jinsi mfumo wa utumwa ulivyozidi kuendelea na kukua, ndivyo mahusiano ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa yalivyozidi kupotea kabisa na tukawa na mfumo wa utumwa halisi.
Vilevile, kukiuka kutoka mfumo wa utumwa hadi mfumo wa ukabaila kulifanyika taratibu na bila shaka kulichukua miaka mingi sana. Ndiyo kwa sababu tunaona kuwa mwanzoni mwa mfumo wa ukabaila tunakuta kuna mahusiano ya mfumo wa utumwa. Jamii ya Waswahili katika ufuo wa bahari wa Afrika Mashariki na jamii zingine Afrika, zilidhihirisha ukweli huu, zilikuwa na mahusiano ya kiutumwa wakati mmoja na mahusiano ya umajumuiuliyokomaa na ya ukabaila.
Na hii ni kwa sababu jamii hizi zilikuwa katika kiwango cha kukiuka kutoka mfumo wa utumwa hadi mfumo wa ukabaila. Kwa maneno mengine, ukabaila wa Waswahili ulikuwa mchanga mno na ulikuwa bado haujakomaa na kuwa ukabaila halisi kama ule uliyokuwa sehemu zingine za ulimwenguni kama Ulaya, Urusi na Asia.
Ni muhimu vilevile kukumbuka kuwa tunapozugumza juu ya mfumo wa utumwa, hatuzungumzii biashara ya utumwa ambayo ilitokea katika karne ya 15 hadi juzi tu karne ya 19. Biashara ya utumwa inadhihirisha jinsi historia inavyokuja kujirudia katika enzi za mwisho wa mfumo wa ukabaila na mwanzoni mwa mfumo wa ubepari, kwani msingi wa ubepari wa USA ni utumwa. Watumwa – watu weusi, Waafrika – ndiyo waliyotumika katika mashamba ya pamba ambayo ndiyo chimbuko cha uchumi wa viwanda vya ubepari wa USA.
Fauka ya haya yote tuliyoyasema hadi sasa, lazima tusisitize kwamba pamoja na ukweli kuwa mfumo mmoja hauwezi kuwa kioo cha mfumo huohuo kila pahali ulimwenguni kutokana na tofauti za kihistoria, kijiografia, kimazingira na kitamaduni kuna mambo mengine ya kimsingi ambayo sharti yapatikane kila pahali kila mfumo mmoja mahsusi unapopatikana. Hivyo, tunaweza kuufafanua ukweli huu kuhusu mfumo wa utumwa.
7. Mfumo wa Utumwa
Mfumo wa utumwa ndiyo mfumo wa kwanza wa kitabaka ambao unajulikana katika historia. Katika mfumo wa utumwa, kulikuwa na tabaka la mabwana kwa upande mmoja na tabaka la matwana (ama watumwa) kwa upande mwingine. Njia kuu ya uzalishaji mali ilikuwa ardhi nayo ilikuwa imemilikiwa na tabaka la mabwana. Ijapokuwa kulikuwa na shughuli zingine za kiuchumi kama biashara, makharakana madogomadogo ya kutengeneza vifaa muhimu vilivyohitajika nyumbani na kwa kilimo, kilimo cha mimea na mifugo kiliendelea kuwa msingi wa uchumi wa jamii hii. Kwa sababu hii, ardhi ndiyo iliyokuwa njia kuu ya uzalishaji mali. Nyenzo za uzalishaji zilikuwa zimekua na kuongezeka mara nyingi sana kulingana na jinsi zilivyokuwa katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Hii ina maana kuwa binadamu katika mfumo wa utumwa walikuwa na uhuru zaidi kutoka kwa maumbile. Yaani, walikuwa wameendelea zaidi katika kuzitawala sheria za maumbile na kuzitumia na kuyafaidi maumbile kwa ajili ya kutosheleza mahitaji yao. Walikuwa wamepiga hatua kubwa sana kisayansi na kitekinologia, na kwa hivyo waliweza kuzalisha utamaduni zaidi kwa wingi na kwa ubora zaidi.
Mazao ya utamaduni na ustaarabu ambayo yanaonekana hata leo na kujulikana kama ustaarabu wa Wamisri, Warumi, Waajemi na Wayunani wa zamani, kwa mfano, yalifanyika katika mfumo wa utumwa. Hivyo, katika mfumo huu watu walikuwa na vifaa na maarifa mengi na bora zaidi kuliko awali. Uwezo huu wa kuzalisha chakula kingi zaidi na mahitaji mengine, utaeleweka vizuri zaidi tukikumbuka kuwa idadi kubwa sana ya watu katika jamii hii, tabaka la mabwana, waliishi bila ya kufanya kazi, walilishwa na kutoshelezewa mahitaji yao yote na watumwa. Hali hii isingeliwezekana hapo awali ambapo nyenzo za uzalishaji hazikuwa zimefikisha jamii katika kiwango hiki cha uzalishaji.
Kuwepo kwa ziada ya chakula na mazao kuna maana kuwa binadamu alikuwa na uhuru wa kuishi muda mrefu zaidi na alikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutekeleza haki zake za binadamu za kuishi kwa amani na furaha zaidi. Kwani hata katika elimu ya matibabu na madawa, kilimo na ufugaji, binadamu alikuwa mbali zaidi kulingana na hapo alipotoka. Pia alikuwa na uwezo wa kujenga nyumba bora zaidi, zilizokuwa na akitekcha ya hali ya juu zaidi, fanicha nyingi na bora zaidi, maridadi zaidi na za kudumu muda mrefu zaidi. Vilevile, binadamu hapa alikuwa akitengeneza vifaa vingi na bora zaidi, nguo bora zaidi, alikuwa na uhuru zaidi wa kusafiri mbali, kuvuka nyika, majangwa, misitu, mito, maziwa na bahari.
Kwa muhtasari, binadamu katika mfumo wa utumwa, alikuwa amezalisha utamaduni halisi zaidi, alikuwa amegundua mengi zaidi, alikuwa akiyatumia na kuyatawala mazingira zaidi kulingana na hapo awali. Na kwa sababu hii alikuwa ameongeza uhuru wake wa kutosheleza mahitaji yake, kustarehe, kujiburudisha, kusafiri, kuwasiliana na kufanya biashara. Aidha, katika kiwango hiki binadamu alikuwa amezalisha utamaduni wa kuwasilisha hisia zake, utamaduni zaidi unaotokana na fikra zake zenye lengo la kujiburudisha, kijijua, kudadisi maumbile na maana ya uhai, na kadhalika. Kulikuwa na falsafa, sanaa mbalimbali na dini ya hali ya juu zaidi kuliko hapo awali. Utamaduni wa mfumo wa utumwa ulikuwa wa kutatanisha na wa upeo mkubwa zaidi kuliko katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Tunasisitiza, katika mfumo huu, binadamu alikuwa na uwezo zaidi wa kutekeleza haki zake za binadamu kuliko hapo awali.
Bali kumbuka tunasema alikuwa na uwezo mkubwa zaidi wala hatusemi alikuwa akitekeleza haki za binadamu zaidi! Hii ni kwa sababu ya ukweli mchungu kwamba siyo binadamu wote waliyofurahia uhuru huu, kwa kuwa mahusiano ya utumwa yalikuwa mahusiano ya kitabaka, ya unyonyaji na unyanyasaji wa mtu kwa mtu.
Tumeona kuwa katika mfumo wa utumwa, nyenzo za uzalishaji zilikuwa zimekua kwa mara nyingi sana kuliko katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa ambao ulitangulia mfumo huo. Hivyo, binadamu kwa ujumla alikuwa huru zaidi kutoka kwa maumbile na alikuwa na uwezo zaidi wa kufurahia na kunufaika na uhuru huo, na wa kutekeleza haki za binadamu zaidi kulingana na hapo awali. Hata hivyo, kukua kwa nyenzo za uzalishaji mali kulileta mahusiano mengine mapya ambayo hayangewezesha watu wote katika jamii hiyo kufurahia uhuru na haki za binadamu kwa usawa.
Kwani wakati wowote ule katika historia, katika mfumo wowote ule wa kitabaka lazima iwe kwamba tabaka moja linafurahia uhuru na haki za binadamu zaidi wakati ambapo tabaka lingine linalazimika kuishi bila uhuru wa kutekeleza haki za binadamu. Aidha, wakati wote, tabaka ambalo linamiliki njia kuu ya uzalishaji mali, huwa ndilo tabaka linalotawala, huwa ndilo tabaka linalokula matunda ya uhuru na kufurahia haki za binadamu, huwa ndilo tabaka lenye ukiritimba wa utajiri na mali na linalofurahia na kufaidi kutoka kwa utamaduni, ndilo linalonyonya, linalogandamiza na kunyanyasa tabaka lingine. Hii ndiyo kanuni ya historia, tabaka mbili haziwezi kamwe kufurahia uhuru na kutekeleza haki za binadamu sawa wakati mmoja. Hilo haliwezekani wala halijawahi kuwezekana katika historia ya binadamu ulimwenguni.
Katika mfumo wa utumwa, tabaka lililonufaika kutoka kwa kukua kwa nyenzo za uzalishaji, tabaka lililokuwa likifurahia uhuru na haki za binadamu, lilikuwa ni tabaka la mabwana ambalo ndilo lililomiliki ardhi, njia kuu ya uzalishaji, ndilo lililodhibiti utajiri wote uliyopatikana katika jamii hiyo. Tabaka la mabwana ndilo lililojipatia haki ya kumiliki kila kitu katika jamii hiyo, hata watumwa wenyewe – binadamu – walikuwa mali ya mabwana kama mifugo yoyote ile. Tabaka la mabwana ndilo lililodhibiti nguvu za dola, ndilo lililokuwa na serikali, polisi, sheria, mahakama, magereza, majeshi, ndilo lililokuwa tabaka la kutawala, kunyonya, kunyanyasa na kugandamiza, ndilo lililokuwa na demokrasi.
Tabaka la mabwana ndilo lililokuwa tabaka la kutumikiwa, kufanyiwa kazi, kuzalishiwa wala halikushiriki katika kazi ya kuvuja jasho ya kuzalisha utamaduni halisi. Chakula, mazao mengine ya kilimo, nguo, majumba, mabarabara, vifaa, vyombo mbalimbali na kadhalika yote haya yalizalishwa na misuli, jasho na kazi ngumu ya tabaka la watumwa. Bali tabaka la mabwana ndilo lililodhibiti, kula na kufaidi matunda yote haya ya utamaduni. Maadamu, halikuwa linafanya kazi ya uzalishaji, tabaka la mabwana lilikuwa na nafasi nzuri ya kufurahia uhuru wa kimawazo. Hivyo, ni tabaka la mabwana ambalo liliongoza katika falsafa, dini, sanaa kama muziki, fasihi, uchoraji na ufinyanzi, na kadhalika. Kwa ufupi, tabaka la mabwana ndilo lililokuwa na uhuru wote uliyokuwako katika jamii ya mfumo wa utumwa. Kwa mfano, tunaposema kuwa Wayunani ndiyo waliowapatia walimwengu neno ”demokrasi“, lazima tukumbuke bila kusahau kwamba tabaka la mabwana – raia – tu, ndilo lililokuwa na hiyo demokrasi, kama vile haki zingine zote.
Kwa upande mwingine, tabaka la watumwa, halikufurahia uhuru ama haki yoyote ile katika jamii ya mfumo wa utumwa. Kwani tabaka la watumwa halikuwa na umilikaji wowote wa njia kuu ya uzalishaji, halikuwa na ardhi, halikuwa na mifugo, halikuwa na vifaa, halikuwa na kitu chochote kile isipokuwa uhai wao tu, nao uhai wao ulitegemea mabwana. Watumwa wenyewe walikuwa mali ya mabwana, na kwa hivyo mabwana zao walikuwa wakiwanyanyasa kwa kila hali na kuwawaua vururumtende. Kwani katika mfumo wa utumwa, mabwana walikuwa huru kuwafanyia watumwa wao chochote kile walichoweza kufanyia mifugo yao, mimea yao na mali yoyote ile.
Watumwa ndiyo waliyozalisha utamaduni halisi, bali hawakuwa na haki ya kula ama kufurahia matunda ya utamaduni huo. Hali ya maisha ya watumwa ilikuwa ni ya kutukanwa, kukemewa, kupigwa, kuteswa, kubakwa, kudhalilishwa, kunyanyaswa na kugandamizwa mbele na nyuma. Wala watumwa hawakuwa na uhuru wa kusema, kuabudu, kutembea, kujumuika, kuburudika, kumiliki mali, hawakuwa na uhuru wowote ule. Watumwa hawakutekeleza haki za kidemokrasi, tabaka la mabwana lilihakikisha kuwa watumwa hawakutekeleza haki yoyote ile isipokuwa tu ile ya kuwawezesha kuwa hai kama watumwa kwa ajili ya kuwatumikia mabwana.
Tumesema kuwa hata huko Uyunani ambapo tulipata neno demokrasi, yaani serikali ya watu, inayoongozwa na watu kwa ajili ya watu, watumwa hawakufikirika kulingana na demokrasi kwani hawakuhesabiwa kuwa watu. Waliyokuwa watu na hivyo na demokrasi ni wa tabaka la mabwana ama raia. Hakika demokrasi ilitumika kuwagandamiza watumwa, dola lilikuwa chombo cha tabaka la mabwana cha kuwanyonya, kuwanyanyasa na kuwatawala watumwa, cha kuendeleza na kudumisha mahusiano ya kitumwa.
Kufikia hapa, ni muhimu tutaje kanuni nyingine muhimu ya histroria, nayo ni, wakati wowote panapokuwa na mfumo wa kitabaka, moja kwa moja kunakuwepo na harakati za kitabaka. Harakati za kitabaka haziwezi kamwe kuepukika panapo mfumo wa kitabaka. Nazo harakati za kitabaka ni mapambano ama makinzani kati ya tabaka linalotawala na tabaka linalotawalwa. Tabaka linalodai mageuzi na lile linalopinga mageuzi. Tabaka linalotawala hutumia dola – serikali, sheria, mahakama, polisi, majeshi, jela, propaganda, dini, na kila mbinu na hila kupinga mageuzi, kuhakikisha litadumu kunyonya na kugandamiza tabaka linalolitawala milele. Kwa maneno mengine, tabaka linalotawala hupora tabaka linalotawalwa haki zao za binadamu.
Nalo tabaka linalotawalwa hupambana na hupigana kwa kila mbinu na hila dhidi ya tabaka linalotawala na dhidi ya dola likiwa na lengo la kuleta mabadiliko ya kuhakikisha kuwa limejikomboa kutoka kwa udhalimu huo na kujishindia haki ya kufurahia uhuru na kutekeleza haki za binadamu.
Kusema kweli, kila hatua iliyopigwa mbele na tabaka linalonyanyaswa katika kujishindia uhuru wao, imepambaniwa. Kila ongezeko la uhuru na utekelezaji wa haki za binadamu ni mazao ya mapambano na vita vikali vya wanaonyanyaswa. Haki haipatikani bure, kila haki hupatikana kwa kupiganiwa. Haijatokea wala haitatokea katika historia kwa wadhulumiwa kukombolewa kwa huruma ama misaada ya wadhalimu wao. Wala hautatokea wakati wowote, leo ama kesho, ambapo wadhalimu watachoka kuwanyonya, kuwanyanyasa na kuwagandamiza wadhulumiwa na wakaamua kuwapa au kuwarudishia uhuru wao na haki zao kwa hiari yao wenyewe.
Wakati wote katika mfumo wa utumwa harakati za kitabaka zilikuwa kali sana. Kila wakati watumwa walipigania ukombozi wao kwa kila njia na mbinu. Walifanya hujuma kama kuharibu mimea na vifaa; kuua mifugo na kutokomeza mali ya mabwana wao; waligoma kufanya kazi; walichoma mashamba na nyumba; walijiua wenyewe; waliwaua mabwana na jamaa zao kisiri na kimachomacho; na mara kwa mara walikula njama wakajizatiti na kuchukua silaha kupigana dhidi ya mabwana na vyombo vya dola. Wakati mwingine walifanya hujuma na kufanya kazi shingo upande au kishaghalabaghala. Kweli walipigania uhuru wao na haki zao kila mara kwa maneno na kwa vitendo na mapambano yao yalijidhihirisha kwa njia na namna tilatila.
Watumwa hawakukubali utumwa, hawakuwa watumwa kwa hiari yao, na ndiyo kwa maana kila wakati dola lilitumika kuulinda mfumo wa utumwa na masilahi ya mabwana na kupinga juhudi za ukombozi wa watumwa.
Wakati huo huo nyenzo za uzalishaji ziliendelea kukua, vifaa na vyombo vipya na bora zaidi vya uzalishaji vikazidi kugunduliwa na kutengenezwa, na uzalishaji ukaongezeka mara nyingi zaidi. Mabwana wakazidi kujilimbikizia ziada kwa utajiri uliyotokana na kazi ya watumwa. Utamaduni ukazidi kukua na kuongezeka kila kuchako.
Bali katika kiwango hiki kukawa na makinzano kati ya nyenzo za uzalishaji na mahusiano ya uzalishaji ya mfumo wa utumwa. Kwa upande mmoja mabwana walihitaji kukua kwa nyenzo za uzalishaji mali ili kuongeza uhuru wao wa kufurahia haki za binadamu, wapate ziada za utajiri zaidi, mazao zaidi, anasa na starehe zaidi, utamaduni zaidi. Kwa upande mwingine, mapambano ya kila mara ya watumwa ya kugomea maisha ya utumwa, kukataa kunyonywa na kunyanyaswa, kutaka kujikomboa, yalizuia kukua kwa nyenzo za uzalishaji, kwani vita vya watumwa, njama zao, hujuma zao na madhihirisho yote ya mapambano yao, tayari yalikuwa yanazuia kuongezeka kwa uzalishaji, kukua kwa vyombo vya kufanyia kazi, kupanuka kwa uchumi, kuendelea kwa sayansi na tekinolojia kwa ujumla. Hali kadhalika, hali ya kulazimika kuwa katika mapambano dhidi ya watumwa kila siku kulipunguza uhuru wao na kuwazuia kuwa na maendeleo ya kutekeleza haki za binadamu. Kwani watumwa hawakuwapatia nafasi hawa wanyonyaji kula manyonyaji yao kwa furaha, amani na utulivu.
Kwa hivyo, ikaanza kuonekana kwa mabwana kuwa ili kuongeza uzalishaji mali na pia uhuru wao, ilipasa kuwe na mageuzi, kuwe na hali ambapo watumwa watawafanyia kazi kwa hiari yao. Kwa maneno mengine, ili nyenzo za uzalishaji ziendelee kukua na ili waendelee kuongeza utekelezaji wa haki zao za binadamu, iliwabidi wabadilishe mahusiano ya kitumwa, wamtambue mtumwa kama binadamu, yaani wampe mtumwa haki yake ya kutambuliwa kama mtu. Kwa muhtasari, iliwapasa wavunjilie mbali mfumo wa utumwa na kuleta mfumo mpya wa mahusiano mapya ya uzalishaji ambayo hayangekuwa kikwazo cha kukua kwa nyenzo za uzalishaji na wakati huohuo, sawia, yaendelee kuhakikisha kuwa mabwana wanaendelea kuwa watawala na wenye kufurahia uhuru na utekelezaji wa haki za binadamu zaidi.
Tumeona kuwa kukua kwa nyenzo za uzalishaji mali katika mfumo wa utumwa, kuliwezesha sehemu ya binadamu, tabaka la mabwana, wenye mali, matajiri, kufurahia uhuru na kutekeleza haki zao za binadamu zaidi kuliko awali. Wakati huohuo, huko kukua kwa nyenzo za uzalishaji kulikoleta mahusiano ya kiutumwa kutoka kwa yale ya kiumajumui, kulifanya binadamu wengi, tabaka la watumwa, kukosa uhuru wao na kuporwa uwezo wa kutekeleza haki zao za binadamu. Yaani, ingawa nyenzo za uzalishaji zilifanya kuwe na uwezo zaidi wa binadamu wote kwa ujumla kufurahia haki zao za binadamu kuliko hapo awali, tunaona kuwa watumwa waliishi maisha ya kishenzi na kinyama, ya kunyonywa na kunyanyaswa, walikuwa katika hali ya kusikitisha zaidi kuliko jinsi binadamu walivyokuwa katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa.
Ni muhimu kukumbuka kuwa kila mara katika mfumo wowote wa kitabaka (na tangu mfumo wa umajumuiuliyokomaa), wanawake kama kundi katika jamii wamekuwa wakinyanyaswa na wanaume. Hivyo, katika mfumo wa utumwa wanawake waliumia kuliko wanaume kwani waligandamizwa maradufu, kama watumwa na vilevile kama wanawake. Aidha, wanawake wa nchi zilizokuwa zikitawalwa na nchi zingine walinyanyaswa kama watuwa, kama wanawake na kama watawaliwa. Hili ni muhimu sana kukumbuka kwa kuwa kiwango cha uhuru wa wanawake katika jamii ni dhihirisho la kiwango cha uhuru wa jamii kwa ujumla. Jamii yoyote ile ambayo inawabagua na kuwagandamiza wanawake haiwezi kamwe kuwa huru. Pia inachelewesha kukuwa kwa hali ya utekelezaji wa haki za binadamu katika jamii huzika.
Katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, sehemu ya binadamu inayojulikana kama wanawake ilinyanyaswa na sehemu ya binadamu inayojulikana kama wanaume. Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kuwa wanawake walinyanyaswa zaidi katika mfumo wa utumwa kuliko katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Kwani katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa wanawake waligandamizwa kama wanawake na wanaume, bali katika mfumo wa utumwa wanawake waligandamizwa maradufu, kama watumwa na tabaka la mabwana na vilevile kama wanawake na wanaume wote kwa ujumla kutoka tabaka zote mbili.
Hii ni kusema kuwa katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa binadamu kwa ujumla walifurahia uhuru na haki zao za binadamu kwa kiasi kikubwa zaidi kufungamana na hali halisi ya mfumo huo ambao haukuwa wa kitabaka, hata ingawa mfumo wa utumwa ulikuwa wa juu zaidi kwa kila hali isipokuwa katika uhusiano wa mtu na mtu. Mfumo wa utumwa ulikuwa na uhuru zaidi bali huo uhuru uliwanufaisha tabaka la mabwana na kuwanyanyasa tabaka la watumwa ambalo lilikuwa la watu waliyolazimika kuishi maisha ya mateso, dhuluma na kinyama kuliko ya binadamu wa awali. Hakujatokea mfumo wowote ambapo binadamu amewahi kuporwa ubinadamu wake kuliko ule wa utumwa.
Tumeona kuwa, mfumo mpya na wa hali ya juu zaidi wa kijamii-kiuchumi unaletwa na mambo mawili muhimu. Jambo la kwanza ni kukua kwa nyenzo za uzalishaji mali kunakosababisha kuongezeka kwa uhuru wa jamii na kufanyika kwa mabadiliko ya mahusiano ya kijamii. Pili ni uwezo wa binadamu wa kuzielewa sheria halisi za maumbile na maendeleo ya kijamii na kuzitumia kuleta mabadiliko, yaani harakati za kitabaka. Kwa mfano, mapambano ya watumwa kila siku ya kujikomboa kutoka kwa utumwa, yalisababisha makinzano ambayo yalileta mfumo mwingine mpya wa hali ya juu zaidi, mfumo wa ukabaila. Hivyo, mfumo wa ukabaila ukakua kutoka kwa mfumo wa utumwa jinsi mfumo wa utumwa ulivyokua kutoka kwa mfumo wa umajumuiuliyokomaa, na jinsi mfumo wa umajumuiuliyokomaa wenyewe ulivyokuwa kiwango cha juu zaidi na cha mwisho cha mfumo wa umajumui. Safari ya uhuru wa binadamu ikawa inasonga mbele, taratibu, kiupogoupogo, kwa migongano na migogoro, kwa milima na mabonde, almradi historia ya binadamu daima huenda mbele na mwendo wake siyo wa msitari uliyonyoka.
8. Mfumo wa Ukabaila
Tulisema hapo awali kuwa wakati ukoloni ulipowasili katika nchi yetu, mataifa ya Kenya ya Waswahili: Mombasa, Lamu, Pate, Malindi, Vanga, Siu, na kadhalika yalikuwa katika kiwango fulani cha mfumo wa ukabaila. Na kwa vile ukabaila wao haukuwa umekomaa, bado kulikuwepo na mahusiano ya umajumuiuliyokomaa na utumwa sambamba na ya ukabaila.
Hata hivyo, mahusiano ya umajumui na utumwa yalikuwa yakimalizika na kupisha yale ya hali ya juu zaidi ya ukabaila. Hii ndiyo hali vilevile ilivyokuwa katika sehemu nyingi za Afrika ambapo kulikuwepo na ukabaila. Ukabaila wa Afrika haukuwa umepevuka na hivyo bado kulikuwepo na mahusiano ya umajumuiuliyokomaa na utumwa pamoja na yale ya ukabaila sambamba na sawia. Basi, wakati tunaendelea kuzungumzia ukabaila katika mataifa ya Waswahili, lazima tukumbuke wakati wote, pamoja na mahusiano ya ukabaila ambayo yalikuwa yakiendelea kukua na kukomaa zaidi, kulikuwepo bado mahusiano ya kiumajumui na kiutumwa ambayo yalikuwa yakiyoyoma na kufa ili kupisha ya kikabalila.
Maadamu mfumo wa ukabaila u mbele ya mifumo yote ya awali kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, yaani nyenzo za uzalishaji katika mfumo huu zilikuwa mbali sana kuliko katika mifumo ya umajumui na utumwa, tunaweza kusema kwa sahihi kuwa, Waswahili walikuwa mbele zaidi kimaendeleo kulingana tuseme na Wadawida, Wamijikenda, Wakikuyu, Wajaluo, Wakalenjin, na makabila mengine ya Kenya.
Waswahili walikuwa wakiishi, (na bado wanaishi) katika ufuo wa Bahari Hindi ya Afrika Mashariki na visiwa vyake, kutoka mpaka wa Kenya na Somalia hadi mpaka wa Tanzania na Msumbiji. Tukizingatia maana ya uhuru tuliyoufafanua mapema katika insha hii, tunaona kuwa Waswahili walikuwa huru zaidi kama mataifa na hivyo walikuwa na uwezo zaidi wa kutekeleza haki zao za binadamu kuliko kabila lolote lingine nchini.
Nyenzo zao za uzalishaji zilizokuwa zimekua sana, ziliwawezesha Waswahili kuzalisha utamaduni halisi wa hali ya juu sana, na ambao ulikuwa wa upeo mkubwa zaidi kuliko wa jamii zingine nchini. Kwa mfano, maendeleo yao katika sayansi na tekinolojia, yaliwawezesha kutengeneza vyombo vya kusafiria baharini kama mitumbwi, ngalawa na mashua. Jambo hili liliwawezesha siyo tu kuwa wavuvi stadi katika Bara Hindi bali pia kuwasiliana na mataifa mengine ulimwenguni na kufanya biashara na kuathiriana kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na hata kidamu. Mamia ya miaka iliyopita tayari Waswahili walikuwa wakisafiri hadi India, Mashariki ya Kati na Uchina. Walikuwa wakifanya biashara na watu wa mataifa haya wakiuziana na kubadilishana bidhaa kama nguo, pembe za ndovu, vifaru, ngozi, mchele, ngano, matunda, viungo vya kukolozea chakula na kadhalika.
Na kwa kuwa Waswahili walikuwa na uwezo mkubwa wa kisilaha na vita, waliweza kutawala biashara ya dhahabu, vipusa na watumwa katika pwani ya Mashariki mwa Afrika kwa miaka mingi sana. Hivyo, mataifa ya Waswahili yaliweza kuwa na utajiri huu pamoja na utamaduni wa hali ya juu wa ukabaila uliowawezesha kuishi mijini. Miji ya Mombasa, Malindi, Takaungu, Lamu, Pate, Siu na Vanga ilikuwako mamia ya miaka iliyopita. Tena miji hii ilijengwa kwa kutumia mipango na akitekcha ya kiwango cha juu kwa wakati wake, ambayo imeiwezesha miji hii (na magofu ya miji hii) kuonekana hadi leo. Hakuna kabila lolote nchini lililokuwa na utamaduni wa kujenga na kuishi mijini wa aina hii Afrika Mashariki. Wala hakuna watu wengine wowote Afrika Mashariki waliyoweza kusafiri mbali zaidi na kuingiliana na kufanya biashara na mataifa ya mbali nje ya Afrika Mashariki, isipokuwa Waswahili. Na hii ni kwa sababu Waswahili siyo tu kijiografia walikuwa wakiishi pwani ya Afrika Mashariki bali pia walikuwa katika mfumo wa ukabaila ambao ni wa juu zaidi kwa kila hali kuliko mfumo wa umajumuiuliyokomaa ambao ndiyo uliokuwa mfumo wa makabila mengi ya Kenya.
Pamoja na hayo, tunajua kuwa kulikuwa na makabila katika bara la Kenya kama Waluhya wa ufalme wa Wanga (Nabongo Mumia) huko Mumiasi ambako leo ni sehemu ya Kaunti ya Kakamega ambao pia walikuwa katika kiwango cha mwanzo cha ukabaila. Ufalme wa Wanga vilevile ulikuwa na dola na utamaduni wa hali ya juu zaidi kiutawala na kisiasa kulingana na makabila mengine nchini. Hata hivyo, ukabaila wa ufalme wa Wanga ambao ulikuwa ikikua na kupanua mipaka yake Magharibi mwa Kenya haukuwa umefikia kiwango cha ukabaila uliyokuwa katika pwani ya Kenya na visiwa vyake.
Nyenzo za uzalishaji za ukabaila, ziliwezesha dola za Waswahili kuwa na tabaka la watu ambao walikula na kufurahia chakula ambacho hawakushiriki katika kukizalisha moja kwa moja. Wakaishi kwa raha mustarehe huku wakiponda anasa kwa uchumi wa biashara na marupurupu peke yake. Kweli walizalisha utamaduni halisi wa hali ya juu, walikuwa na fanicha na vyombo vya hali ya juu, vyombo vya kulia vya udongo, shaba na chuma, mapambo na nakshi tilatila, nguo, vyakula vya aina nyingi na mapishi ya kumtoa nyoka pangoni, ala za muziki, silaha, na kadhalika. Mazingira yao ya kuwa katika Bahari Hindi, na uwezo wao wa kutekeleza uhuru wa kusafiri mbali uliwawezesha kuingiliana na kuathiriana na Waarabu, Waajemi, Wahindi, Wayahudi, Wachina na baadaye Wazungu. Hili liliwawezesha kujifunza maarifa mengi na kunufaika kutoka kwa tamaduni za watu wengine. Haya yote yalisaidia kuongeza uhuru wao.
Uwezo wao wa kuwa na mataifa thabiti, dola, silaha, utamaduni wa ukabaila kwa ujumla, uliwawezesha kulinda uhuru wao (na wa Kenya kwa ujumla) kutoka kwa uvamizi wa wageni kama Waarabu na Wareno. Kwa mamia ya miaka Waswahili wa Mombasa, Malindi, Lamu na Pate walipambana kwa ushujaa kulinda heshima ya mtu mweusi na kupinga kutawalwa na kunyonywa na wageni. Kwa mfano, Wareno walishindwa kutawala Waswahili na kwa njia hii hawakuweza kupenya na kutawala bara la Kenya jinsi walivyofanya Msumbiji, Angola, Guinea Bissau, Principe na Sao Tome, kwa vile utamaduni wa Waswahili wa ukabaila uliwawezesha kujihami bora zaidi. Kwa miaka mingi Waarabu walishindwa kuwatawala Waswahili, na walipofaulu ilikuwa ni kwa muda mfupi tu, tena huko kulitokana siyo na kuwashinda kivita moja kwa moja, bali kutokana na mbinu zingine kama za dini ya Kiislamu, kuchochea na kudhamini vita kati ya falme za Mombasa na Malindi na Lamu na ujanja wote wa wafalme wa Oman. Tena hakuna wakati wowote Waswahili wote, waliinua mikono na kukubali kutawalwa na Waarabu, waliupinga utawala wa kigeni siku zote.
Kwa muhtasari, kutokana na kuwa katika mfumo wa ukabaila, uliyozalisha nyenzo za uzalishaji za hali ya juu zaidi kuliko awali, na kusababisha kuwepo kwa mataifa, dola na utamaduni mkubwa na wa upeo mpana kwa kila hali, Waswahili walifaulu kujitetea na kupigania haki yao ya binadamu ya kujitawala na kujiamulia sudi yao wenyewe kama taifa kwa muda mrefu. Aidha, waliweza kuwazuia wageni kupenya na kuvamia bara la Kenya kwa miaka mingi.
Tukikumbuka haya yote, tutaelewa kwa nini ilichukua muda mfupi kwa Kenya kutawalwa na Wingereza wakati ambapo Waswahili waliupinga uvamizi wa wageni kwa karne nyingi. Kwanza Waingereza walikuwa katika mfumo wa ubepari ambao kama tutakavyoona, ulikuwa wa hali ya juu mno kulingana na mfumo wa umajumuiuliyokomaa uliyokuwa historia ya makabila mengi ya Kenya kama tulivyokwisha kuona. Waswahili walikuwa na mataifa yaliyokuwa na dola na vyombo vyote vya dola1. Kwa sababu hii walikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kujihami na kutetea uhuru wao. Kwa upande wao makabila mengi ya Kenya yaliyokuwa katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa hayakuwa mataifa bali koo na mbari mbalimbali na yalipolazimika kuupinga ukoloni, yalifanya hivyo bila kushirikisha ama kupata msaada wa koo au mbari zingine ama makabila mengine. Hili lilichangia katika kuwafanya wadhaifu dhidi ya ukoloni. Ni muhimu tusisitize kuwa wakati ukoloni ulipowasili, hatukuwa Kenya, tulikuwa katika kiwango cha mbari na makabila. Taifa la Kenya lilizaliwa baada ya ukoloni kuwasili. Aidha, mfumo wa ukabaila wa Waswahili uliwawezesha kuwa na uwezo wa mpangilio wa kisiasa, kisilaha na kijeshi wa hali ya juu zaidi kuliko ule wa makabila ya bara la nchi yetu. Hakika ilikuwa vigumu zaidi kwa ukoloni kuwatawala Waswahili ambao walivamiwa na ukoloni wakiwa katika mfumo wa ukabaila kuliko makabila mengine ya nchi yetu ambayo yalikuwa katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa2.
Kabla hatujaendelea inafaa hapa tusisitize kuwa popote duniani, nyenzo za uzalishaji za mfumo wa ukabaila ziliwezesha kujenga utamaduni wa ustaarabu wa hali ya juu: miji, majumba, mabarabara, vyombo vya usafiri vya hali ya juu, biashara, na kadhalika. Maajabu ya duniani kama makasri, majumba ya kidini, misikiti, makaburi na mapiramidi, mengi yana historia yake katika utumwa-ukabaila. Utumwa – ukabaila vilevile ulizalisha dini kuu za ulimwengu, kama Uyuda, Ukiristo, Uislamu, Uhindu, Uzorosta na Ubudha, ulizalisha falsafa, sanaa, uandishi wa hali ya juu. Kulingana na upeo wa mada yetu, hatutazama zaidi kuzugumza kuhusu mfumo wa ukabaila kwa undani. Tunachotaka kukifanya ni kusisitiza tu kuwa ukabaila ulikuwa mbali sana mbele kwa kila hali kulingana na mifumo yote ya hapo awali. Hivyo, katika mfumo wa ukabaila jamii ilikuwa huru na uwezo wa kutekeleza haki za binadamu zaidi kuliko kwa mfano katika mfumo wa utumwa ama wa umajumui.
Hata hivyo, hadi sasa tumesema kuwa mataifa ya Waswahili kwa ujumla yalikuwa huru zaidi, na yalikuwa na uwezo zaidi wa kutekeleza haki za binadamu kuliko makabila mengine ya Wakenya kwa kuwa nyenzo za uzalishaji katika mfumo wa ukabaila zilikuwa za hali ya juu zaidi. Bali lazima tukumbuke kuwa mfumo wa ukabaila ulikuwa mfumo wa kitabaka na tumesisitiza kuwa katika mfumo wa kitabaka lazima kuwe na tabaka moja linalofurahia uhuru na kutekeleza haki za binadamu zaidi kuliko tabaka lingine.
Hivyo katika mfumo wa ukabaila kulikuwa na tabaka la makabaila na tabaka la wajoli. Tabaka la makabaila lilikua kutoka kwa tabaka la mabwana, nalo ndilo lililomiliki na kudhibiti njia kuu za uzalishaji mali, ardhi. Ndilo lililokuwa na mifugo, vyombo vya uzalishaji, ndilo lililotawala biashara na uchumi wote wa jamii kwa ujumla.
Kwa kuwa lilimiliki na kudhibiti njia kuu za uzalishaji, tabaka la makabaila liliweza vilevile kudhibiti na kufurahia matunda ya uhuru, utamaduni na kutekeleza haki za binadamu zilizowezekana kutekelezeka wakati huo. Lilifanya haya yote kwa kunyonya, kunyanyasa na kugandamiza tabaka la wajoli lililozaliwa na tabaka la watumwa na ambalo katika ukabaila halikuwa na umilikaji wa njia kuu ya uzalishaji, ardhi.
Tabaka la makabaila liliishi maisha ya anasa na starehe, maisha ya umwinyi, maisha ya uvujaji, lilifurahia chochote kizuri kilichozalishwa na ukabaila. Ndilo lililokuwa tabaka la wafalme na mamalikia, ndilo lililokuwa tabaka la wenye mali na walimbikizaji wa utajiri wa kila aina, ndililo lililokuwa na fursa na wakati wa kuwaza na kufikiria kuhusu ulimwengu na malimwengu – na hata mbingu, kwa hivyo ndilo lililozalisha falsafa, fasihi, na sanaa maarufu ya kabla ya karne ya ishirini ya Lamu, Pate, Siu, Vanga, Lamu – ya Waswahili. Tabaka la makabaila ndilo lililokuwa likiongoza jamii katika dini, ndilo lililokuwa na mashekhe na watawa wa kuhubiri dhidi ya maovu duniani na kuhusu ufalme wa mbiguni wa milele na milele amina. Ndilo lililodhibiti nguvu za dola, ndilo lililoshiriki katika siasa na demokrasi, ndilo lililokuwa na uhuru wa kusema, kuabudu, kuandika, kusafiri, kustarehe na kila uhuru uliyokuwa ukiwezekana nyakati hizo. Ndilo tabaka lililokuwa likitawala biashara na kutengeneza sera za mahusiano na mataifa mengine. Hili ndilo tabaka lililokuwa likisababisha vita dhidi ya mataifa mengine, ndilo lililokuwa likipiganiwa kwa jina la ’uhuru wa taifa letu’, kwani kwenye ukabaila taifa liligawanyika kitabaka kati ya taifa la makabaila na la makabwela na wajoli. Tabaka hili la makabaila liliishi kwa uzembe na ulegevu, kwa umwinyi, kwa raha mustarehe, kwa kufanyiwa kazi, kwa jasho la wajoli na watumwa.
Tabaka la wajoli lilikua kutoka kwa tabaka la makabwela na watumwa. Tuliona jinsi migongano kati ya nyenzo za uzalishaji na mahusiano ya uzalishaji yalivyosababisha, hatimaye, kuzaliwa kwa mfumo wa ukabaila kutoka kwa ule wa utumwa. Tumeona pia jinsi harakati za kitabaka za watumwa za kupigania uhuru wao, zilivyolazimisha mabwana kuwapa watumwa uhuru zaidi. Hivyo, mabwana wakalazimika kuwarudishia watumwa wao haki ya kuhesabiwa kama binadamu.
Kwa sababu hii, kulingana na mtumwa ambaye hata hakuwa anahesabiwa kama mtu, wajoli walikuwa huru zaidi kwani angalawa sasa katika ujoli walihesabiwa kama watu, hata ingawa ni kwa maneno tu. Bali kwa vyovyote vile, wajoli walikuwa mbali sana na ukombozi kwani walipopata uhuru huo kutoka kwa utumwa mabwana walihakikisha kuwa hawakuwa na njia ya kujipatia riziki, hawakuwa na umilikaji wa ardhi, hawakuwa na vifaa, hawakuwa na chochote kile isipokuwa mili yao tu. Watumwa hawakuwa na umilikaji wa njia ya uzalishaji. Ndiyo kwa maana hawakuwa na haki juu ya uhai wao, kwani ili kuwa hai lazima uwe na chakula, nacho chakula huzalishwa kutoka kwa ardhi na wajoli hawakuwa na ardhi. Ardhi yote ilimilikiwa na mabwana ambao sasa ni makabaila.
Hii ndiyo ilikuwa hali ya wajoli. Na katika hali hii iliwapasa waendelee kuwategemea makabaila kwa haki yao ya uhai maana makabaila walihakikisha kuwa watumwa walitambuliwa kuwa watu lakini watu wasiyo na umilikaji wa njia kuu ya uzalishaji. Kwa njia hii wajoli wakafungwa na makabaila kwa ukabaila na wakaendelea kunyonywa na kunyanyaswa katika maeneo waliyoishi. Makabaila waliwakodisha ardhi kwa masharti kwamba wakubali kuwapatia (makabaila) mazao yote ya ardhi hiyo isipokuwa kiasi kidogo tu cha kuwaweka hai ili waendelee kuwalimia na kuwazalishia makabaila. Iliwapasa wajoli waendelee kuwatii makabaila na sheria zao za kidhalimu, la sivyo watanyang’anywa njia ya uhai, ardhi.
Ndipo ikawa kwamba tabaka la wajoli ndilo lililozalisha utamaduni wote halisi: chakula, mifugo, vyombo vya uzalishaji na vya nyumbani, majumba, mabarabara – kila kitu, bali halikufurahia hata kidogo utamaduni huo wa jasho lao. Tabaka la wajoli ndilo tabaka lililokuwa msingi wa uhai bali ndilo lililokuwa na haki ndogo zaidi kuwa hai. Maisha ya wajoli yalikuwa ya kufanya kazi, njaa, dhiki tilatila, ukosefu, ukiwa, uchungu, uchochole, kudhulumiwa na ya kinyama. Wajoli wakawa hawana uhuru wa kutekeleza haki zao za binadamu.
Lakini, wajoli hawakuupenda wala hawakuukubali ukabaila. Hawakukaribisha kunyonywa, kugandamizwa na kudunishwa. Hawakupendelea kuporwa haki zao na makabaila. Ushahidi madhubuti wa kihistoria unadhihirisha kuwa kila wakati katika historia ya ukabaila ulimwenguni kulikuwako na harakati za kitabaka kali sana ambazo zilijidhihirisha kwa namna mbalimbali. Wakati wote wajoli waliupinga ukabaila na kupigania uhuru na ukombozi wao kwa maneno na kwa vitendo kwa kutumia njia mbalimbali.
Makabaila walilazimika kila mara kuzidisha na kuimarisha nguvu za dola, yaani serikali, polisi, sheria na mahakama, majeshi na magereza katika juhudi za kuhifadhi, kuendeleza na kuimarisha mfumo huu wa kidhalimu. Mamilioni ya wajoli walikamatwa, waliteswa, walifungwa na kuuawa na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya ufalme na ukabaila. Sheria za uchochezi za kupinga uhuru wa kusema, kujumuika, kuandika, kutembea, kukosoa serikali na zilizokusudiwa kuimarisha utamaduni wa hofu na kimya zilitumika sana dhidi ya wajoli.
Kila pahali palipokuwepo na mfumo wa ukabaila duniani, watu wanaojulikana kama wafalme, mamalkia, masultani, matzar, mashah, makabaka, manabongo, making, maqueen, na kadhalia, kulingana na nchi tofautitofauti, walikuwa jazanda na taswira za utawala wa imla, ukiritimba wa uchumi, udhalimu, unyama, ubadhirifu, ulafi wa mali, unafiki, uzembe, ufisadi, umwinyi, kiburi – adili ya kikabaila. Wafalme walikuwako ili kudhibiti dola la kulinda masilahi ya tabaka la makabaila na mfumo wa kikabaila na kuhakikisha kuwa tabaka la wajoli linatii amri za makabaila na utawala wa kiimla wa kisultani (ama wa kikabaka, kishah – almradi makupe hawa wana majina chungu nzima ambayo unaweza kuwaita).
Aidha, makabaila waliwapiga wajoli vita vya kipropaganda na kisaikolojia vilivyokusudiwa kuwafanya waukubali ukabaila, wavumilie udhalimu wa wafalme na makabaila, waogope kupambania ukombozi wao na wawapatie nafasi wadhalimu wao ya kuwanyanyasa kwa amani. Dini ilitumika sana kwa madhumuni haya. Ilihubiri kuwa kila mtu ana kudura yake na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba matajiri na maskini, makabaila na wajoli na kwamba hali hii haiwezi kubadilishwa na binadamu. Dini iliwafundisha wajoli kuwa ni dhambi kuasi ukabaila na ikawapa matumaini ya kuwa na furaha tu baada ya kifo. Ndiyo kwa maana hadi wa leo wanamapinduzi wa kisoshalisti husema kwamba dini ni kasumba ya umma, maana inawafanya umma kulewa na kukosa uwezo wa kupambania ukombozi wao.
Bali katika mapambano yao, wajoli vilevile walipinga propaganda, adili, dini na itikadi zote za makabaila zilizokusudiwa kudumisha mahusiano ya kikabaila. Walijizatiti kwa kutumia itikadi na adili yao wenyewe ya mapambano na ukombozi. Kwa mfano, mabwana na makabaila walifundisha ati heshima si utumwa lakini watumwa na wajoli wenye mwamko walifundisha utumwa si heshima.
Hakuna chochote kile kilichowazuia wajoli wenye mwamko kupigania haki zao, si kuteswa, si kufungwa, si kufanywa wakimbizi, si kunyongwa, si kuuawa kinyama, haya yote hayakuwawezesha wafalme na makabaila kufurahia uhuru wao na haki za kula manyonyaji kwa amani siku zote. Njaa ya uhuru, kiu cha haki za binadamu, matumaini ya ukombozi na maisha bora ya kiutu, haya yote yalidai kutoshelezwa kwa vyovyote vile. Wajoli, kina yahe, wasomi wa kimaendeleo, wapenda haki na demokrasi na wanamapinduzi hawakusita hata siku moja kupambania mageuzi. Wote hawa waliunga mkono wajoli kupigana dhidi ya mfumo huu wa kidhalimu. Wapenda mabadiliko wote waliungangana dhidi ya dola la makabaila na wafalme.
Wakati huu huohuo, nyenzo za uzalishaji ziliendelea kukua, na hata zikafikia kiwango cha juu sana hasa huko Ulaya Magharibi katika karne ya kumi na nne ambapo ukabaila ulikuwa umekomaa na kufikia kilele chake katika karne ya kumi na tisa. Uhuru wa binadamu ulikuwa umekua na kufika kiwango kikubwa sana, hivyo kwamba kulikuwa na ugunduzi wa kasi uliyosababisha maendeleo makubwa katika sayansi na tekinolojia. Na hiyo tekinolojia iliwawezesha watu kutengeneza vifaa na vyombo tilatila vya kitamaduni vya hali ya juu sana. Hii ina maana kuwa uzalishaji mali uliongezeka mara nyingi zaidi kulingana na mifumo ya hapo awali. Utajiri na ulimbikizaji mali ukazidi kuongezeka katika jamii.
Uwezo wa kutengeneza vyombo vya kusafiria katika ardhi na majini, uliongeza sana uhuru wa watu wa kusafiri mbali. Meli, ujuzi wa kusafiri baharini, na silaha za hali ya juu kama bunduki na mabomu, yaliyawezesha Wazungu kutoka Uhispania, Ureno, Uholanzi, Wingereza na Ufaransa kusafiri hadi makontinenti ya Afrika, Amerika, Asia, Australia na New Zealand. Hii ina maana kuwa biashara ya ulimwengu iliongezeka sana na makabaila wa Ulaya Magharibi wakaweza kulimbikiza mabilioni ya pesa na utajiri mkubwa kutoka kwa kuwanyonya wajoli nyumbani na kutoka kwa kuvamia, kutawala, kuwapunja na kupora watu wa Afrika, Asia, na Amerika. Kwa kutumia biashara ya utapeli, kudaganya, kuibia na kupunja watu wa makontinenti mengine, makabaila wa Ulaya walizidi kujilimbikizia mali huko kwao.
Historia ya kipindi hiki na jinsi Wareno, Wahispania, Waholanzi, na baadaye Waingereza, Wafaransa na Wajerumani walivyotumia meli na uwezo wao wa kisilaha, kusafiri na kuvamia, kuua, kutawala, kunyonya na kupora mataifa mengine katika biashara ya uhange na unyama iliyokuwako kati ya karne ya 14 na ya 17 inayojulikana na kila aliyesoma historia ya ulimwengu. Biashara kuu ya viungo vya kukoka chakula, dhahabu, pembe za ndovu, nguo, mapambo na manukato na watumwa, iliwawezesha wafanyibiashara wa Ulaya kulimbikiza utajiri mkubwa huko nyumbani kwao Ulaya kwa kusababisha mamilioni ya watu kuangamia, kuteseka, kukosa makao, kuishi kwa hofu na wasiwasi na kuharibiwa utamaduni wao waliuojenga kwa maelfu na maelfu ya miaka.
Wakati huohuo, sayansi na tekinolojia ilikuwa inahakikisha kuwa ufundi unakua kutoka nyumba za watu binafsi na kupanuka hadi kuwa makarakhana madogo, hata kufika karne ya 18 tayari viwanda vyenyewe vilianza kuonekana, hasa viwanda vya nguo katika pahalai kama Manichester huko Uingereza. Mapinduzi ya kiviwanda yakaenea Wingereza, Wilaya na sehemu zingine kama Japan. Maendeleo haya na nyenzo za uzalishaji yalianza kuzaa tabaka lingine lipya ambalo halikuwako hapo awali, tabaka la wenye viwanda na wafanyibiashara, tabaka la mabepari – kweli kipindi hiki cha historia kilichojulikana kama mwamko ama zinduko, kililipua maendeleo kwa kila nyanja, tangu kilimo na viwanda, tangu fasihi, muziki, uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, uhandisi, sayansi na ugunduzi na kila aina ya sanaa ilinoga na kunawiri. Mabingwa wa fikra za kisanaa za kimaendeleo, wasomi, wanasayansi, wahandisi, wagunduzi na watafiti wa kila aina walijitokeza kwa wingi na kwa ari na ghera ya kupinga mawazo ya awali ya kishenzi, kishirikina, kikabaila na ya kupinga mageuzi. Badala yake wakasambaza mawazo mapya ya kimaendeleo yaliyodai mabadiliko, uhuru, demokrasi na haki za binadamu.
Kwa njia hii mfumo wa ukabaila uliendelea kupigwa vita na kila siku ukazidi kuonekana kuwa unazuia juhudi za binadamu za kukuza uhuru wake na kuzidi kutekeleza haki za binadamu. Wanasayansi nao wakajitokeza na kufanya ugunduzi uliyozidi kuongeza uwezo wa binadamu wa kuzifahamu, kuzitawala na kuzitumia sheria za maumbile kwa ajili ya kuongeza uhuru wa binadamu. Sayansi ikatafsiriwa katika tekinolojia na kuleta vyombo vya uzalishaji vya kila aina, vifaa vipya na mashini ambazo hazikuwahi kuonekana katika historia ya binadamu.
Katika kiwango hiki pia, wajoli, wakulima wachochole na maskini na makabwela kwa ujumla, walizidisha mapambano yao dhidi ya udhalimu wa makabaila na wafalme wakiungwa mkono na mkondo wa historia kama tulivyoona. Nalo tabaka lililokuwa likitokota na kuchipuka, la wenye kumiliki uchumi wa viwanda na biashara, tabaka la mabwanyenye, likazidi kuona kuwa mfumo wa ukabaila ulikuwa unapinga kukua kwa biashara na viwanda vyao. Wanafunzi, walimu na wasomi, kama makabaila na wajoli, pia walitambua kuwa ukabaila na ufalme ulikuwa kikwazo cha maendeleo ya kitamaduni, kisayansi, kisanaa na kidemokrasi.
Kupanuka kwa viwanda vya mabepari kulihitaji nguvukazi. Na tabaka peke yake ambalo lingewapatia mabepari nguvukazi lilikuwa tabaka la wajoli. Bali ukabaila na sheria za kikabaila zilihakikisha kuwa tabaka hili la wajoli halikuwa na uhuru wa kutembea, uhuru wa kujumuika, uhuru wa kusema, uhuru wa kufanya kazi popote lilipotaka – wajoli hawakuwa na uhuru wowote ule chini ya sheria za ufalme na ukabaila. Wajoli walifungiwa katika mashamba ya makabaila na wakawa hawana uhuru wa kusafiri hadi mijini na kuajiriwa kazi huko. Hivyo, tabaka mpya la mabepari likaona kuwa mapambano ya wajoli na wachochole yalikuwa ya haki na ya kimaendeleo na basi wakaunga mkono mapambano dhidi ya ukabaila na ufalme. Kwa jina la uhuru, usawa, demokrasi na haki za binadamu, tabaka la mabepari likawa kitu kimoja na tabaka la wajoli na kina yahe kuupinga ukabaila na kupigana dhidi ya mfumo huu uliyokuwa kikwazo kwa uhuru na maendeleo ya kijamii. Ilikuwa wazi kuwa mfumo wa ukabaila ulikuwa umepitwa na wakati. Ulikuwa na mimba pevu ya mfumo mpya iliyokuwa tayari kuzalishwa na mkunga wa mapinduzi. Nazo harakati za kimapinduzi – za wajoli, wakulima makabwela, wasomi, wanafunzi, wafanyibiashara, wenye viwanda na matabaka na makundi yote yaliyokuwa yakinyanyaswa dhidi ya mfumo wa ukabaila kupitia kwa wafalme na mamalkia, viongozi wa kidini na makabaila na dola lao – zikazidi kupamba moto.
Ndipo ikatokea katika karne ya kumi na tisa, huko Ulaya, juhudi za pamoja za wajoli na mabepari, kwa harakati za kimapinduzi zikaangusha dola za kikabaila na utawala wa wafalme. Bali haya mapinduzi yakajulikana kuwa mapinduzi ya kibwanyenye kwani tabaka lililochukua nguvu za dola, kisiasa na kiuchumi lilikuwa tabaka la mabwanyenye (mabepari).
Tukumbuke kuwa mapinduzi ni mabadiliko kamili ambapo tabaka moja linanyakua nguvu za dola kutoka tabaka lingine. Ingawa mapinduzi ya kibepari yaliletwa na muungano wa matabaka mbalimbali yaliyokuwa yakipigania uhuru na ukombozi kutoka kwa tabaka la makabaila hatima yake yalikuwa mapinduzi ya kibepari kwani tabaka lililochukua na kudhibiti dola na kulitumia kulinda masilahi yao ya kiuchumi, kisiasa na hata kitamaduni lilikuwa tabaka la mabepari.
9. Mfumo wa ubepari
9.1. Historia ya mfumo wa ubepari
Kumbe tabaka mbili tofauti haziwezi kamwe kuwa na uhuru sawa wakati mmoja, haziwezi kufurahia haki za binadamu sawa sambamba wala haziwezi kuwa na masilahi na malengo mamoja. Hii ni kanuni nyingine halisi ya historia.
Mabepari walipambana dhidi ya mfumo wa ukabaila na dhidi ya utawala wa wafalme kwa kuwa mfumo huu ulikuwa kikwazo kwa nyenzo za uzalishaji walizozihitaji sana katika makharakana na viwanda vyao, ili kuongeza faida na utajiri wao, na ili kupanua biashara zao, mtaji wao. Hali kadhalika waliunga mkono mapambano ya wajoli ya kujikomboa kutoka kwa ukabaila, kwa kuwa walitaka sheria za kidhalimu na za kupinga maendeleo, zilizokuwa zinawafunga wajoli mashambani katika miliki za makabaila ziondolewe na wajoli wawe huru kutembea na kuingia mijini ili waajiriwe na kutumika katika viwanda vya mabepari. Makampuni na mafaktori ya mabepari yalihitaji sana nguvukazi, nayo hiyo nguvu kazi ingepatikana tu kutoka tabaka la wajoli, na hii ingewezekana tu baada ya mfumo wa ukabaila (ambao ulikuwa kizingiti cha maendeleo) kukwamuliwa na badala yake kukuwepo kwa mfumo mpya ambao ungewezesha kukuwepo kwa uhuru wa kuendeleza nyenzo za uzalishaji na wakati huohuo kuwawezesha mabepari kuchukua nafasi ya makabaila kisiasa, kiuchumi, kiutawala na kwa kila hali.
Tumeona kuwa wajoli, kwa upande wao, walipambana vikali dhidi ya ukabaila na ufalme ili kujinyakulia uhuru wao waliyokuwa wameporwa kwa karne nyingi; ili wawe na demokrasi na haki za binadamu; ili wawe na ardhi na maisha bora yasiyo ya kunyonywa, kufukarishwa na kulazimishwa kuishi kama wanyama wa kufugwa. Hata hivyo, mapinduzi ya kibepari ambayo wajoli walishiriki kuyaleta kwa kiasi kikubwa zaidi, bali yaliyoongozwa na mabepari na mabepari-uchwara, yalileta demokrasi ya kibepari inayozungumza kuhusu usawa katika sheria, uhuru wa kutembea, kusema, kusoma, kuabudu, kujumuika, kupiga kura, kumiliki mali na hayo yote ambayo yaliandikwa na yameandikwa kwa katiba za kibepari.
Sasa baada ya mapinduzi ya kibepari, wajoli walijishindia uhuru zaidi, walikuwa huru zaidi kuliko jinsi walivyokuwa chini ya ukabaila. Bali hawakuwa na njia yoyote ya kujipatia riziki, hawakuwa na ardhi, hawakuwa na viwanda, hawakuwa na biashara, hawakuwa na pesa, hawakuwa na chochote kile isipokuwa mili yao tu, isipokuwa uwezo wao wa kufanya kazi – isipokuwa nguvukazi yao tu. Kwa sababu hii, hawakuwa na budi ila kukimbilia mijini kuuza nguvukazi yao kwa viwanda vya mabepari. Wakageuka kutoka kuwa wajoli wa kuzalishia makabaila na kuwa wafanyikazi wa kumenyeka katika viwanda vya mabepari. Na kwa kuwa hawakuwa na chochote kile cha kutegemea kwa riziki yao isipokuwa misuli yao na jasho lao lililowaletea ujira duni, wakaitwa maproletarii na wakawa wanaishi maisha ya maproletarii mijini.
Nayo maisha ya maproletarii yalikuwa maisha magumu, ya kinyama, ya dhiki na kusaga meno, ya njaa na ukosefu, mitaa ya mabanda, ulevi na umalaya, umaskini, ufukara na sulubu, ya hofu na wasiwasi. Yalikuwa maisha ya kufanya kazi kama punda na kuchukuliwa kama punda. Yalikuwa maisha hatari ya kuyumbayumba na ya hofu na dukuduku kuhusu kesho, maisha ya mitaa ya mabanda, maisha yaliyokuwa mbali sana na uhuru na haki za binadamu. Haya ndiyo maisha waliyoishi wafanyikazi huko Wingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Ulaya yote, na pahali popote ubepari ulipojitokeza. Fredrick Engels katika kitabu chake Hali ya Tabaka la Wanyakazi Wingereza (The Conditions of the Working Class in England) amesimulia maisha ya wafanyikazi na maproletarii katika Wingereza kwa marefu na mapana wakati huo.
Waliyokula na kufurahia zaidi matunda ya ugunduzi, sayansi na tekinolojia yaliyoletwa na ubepari, waliyofaidi zaidi kutoka kwa kukua kwa nyenzo za uzalishaji na kuendelea kutekeleza haki za binadamu, walikuwa ni mabepari, matajiri, wenye mali, wafanyibiashara wakuu, mamilionea waliyomiliki njia kuu za uzalishaji katika mfumo wa ubepari – biashara na viwanda.
9. 2. Demokrasi ya kibepari
Ni kweli, mfumo wa ubepari ulijivunia uhuru, demokrasi na haki za binadamu. Hata watu wengi Kenya wanaopambania uhuru, demokrasi na haki za binadamu, wanapambania demokrasi ya kibwanyenye tu! Ukiwauliza watu wengi kuhusu maana ya demokrasi watakwambia wanataka Kenya iwe na hali kama iliyoko USA, Canada, Wingereza, Ujerumani, Japan, Ufaransa na nchi zingine za kibepari za Ulaya Magharibi. Wachache – vibaraka wa mabepari wanaotawala pamoja na mabepari-mchwara – wanaamini na kuelewa kuwa demokrasi inayoweza kutetea masilahi yao ni demokrasi ya kibepari, kwa kuwa wanalenga kuendelea kuwa na hali ya hewa ya kujitajirisha kwa kuwanyonya, kuwarubuni na kuwasaliti umma wa Kenya. Lakini idadi kubwa ya Wakenya, wakulima makabwela na wafanyikazi na mafukara, mawazo yao kuhusu demokrasi yanatokana na kudaganywa na propaganda za kibepari. Wanafundiswa kuwa kilele cha demokrasi ni ubepari kama wa USA, Japan na Ulaya Magharibi, kuwa ubepari ni sawa na demokrasi na demokrasi ni sawa na ubepari. Ati demokrasi ya kibepari ndiyo alfa na omega ya demokrasi. Wakati huo huo wanadanganywa kuwa hapawezi kamwe kuwa na demokrasi katika ukomunisti, eti ukomunisti ni udikteta na udikteta ni ukomunisti! Hizi ndizo propaganda za ubepari kuhusu uhuru na haki za binadamu. Lakini, je, ukweli uko wapi? Ni nini maana ya demokrasi ya kibepari?3
Wafanyikazi (maproletarii) hawakuchukua muda kugundua ukweli kuwa demokrasi ya kibepari ilikuwa demokrasi ya mabepari wala siyo ya watu wote kama walivyokuwa wakifikiria. Katika mfumo wa ubepari, demokrasi, uhuru na haki za binadamu ni matunda ya kufurahiwa na mabepari, matajiri, wenye mali na wala siyo na wafanyikazi, mafukara, wachochole, wavujajasho. Kwani katika ubepari, demokrasi ni serikali ya mabepari inayoongozwa na mabepari kwa ajili ya mabepari na inayolindwa na dola la kibepari.
Katika mfumo wa ubepari, dola ni chombo cha tabaka la mabepari cha kunyonya, kunyanyasa na kutawala tabaka la wafanyikazi, wakulima makabwela na wananchi wote wasiyo na umilikaji wa njia za uzalishaji mali mkiwemo viwanda, biashara kuu na maliasili. Kila wafanyikazi walipojumuika, wakajizatiti na kugoma ama kuandamana kupigania haki zao, vyombo vya dola kama polisi, sheria, jela, majeshi na serikali vilitumiwa kuvunja migomo yao na kupinga masilahi yao. Wakati huohuo waliona vyombo vya dola kila wakati vikitumika kulinda masilahi ya waajiri (mabepari) dhidi ya waajiriwa. Wasomi na wakereketwa waliyokuwa wakifundisha mapinduzi ya kisoshalisti tangu enzi za kina Karl Marx, Fredrick Engels, Vladmiri Lenin na kadhalika walikuwa wakinyanyaswa kwa kila hali na wengi wakafanywa kulazimika kupigania mageuzi kwa kutumia mbinu za chini kwa chini na mara nyingi kutoka magerezani na uhamishoni.
Mabepari hudai ati watu wote katika taifa lao la kidemokrasi wako sawa chini ya sheria. Bali ukweli ni kuwa tabaka linalotunga sheria hizo ni tabaka la mabepari nazo hizo sheria ni za mabepari za kulinda mungu wa ubepari anayeitwa mali ya binafsi au mtaji, zinalinda udikteta wa mabepari – wa matajiri – dhidi ya wafanyikazi na wale wengi ambao ni mafukara wasiyo na umilikaji wa njia kuu za uzalishaji. Isitoshe, haki huuzwa katika ubepari kama bidhaa yoyote ile, kwa kuwa ili kutetewa na wakili lazima utoboke kiasi kikubwa cha pesa. Naye anayeweza kununua huduma za wakili ana uwezo zaidi wa kufaulu katika kesi ama kwa mambo yoyote yanayohusu sheria kuliko yule anayelazimishwa na ufukara wake kujitetea mwenyewe. Hivyo, wenye mali, ambao wana uwezo wa kununua mawakili bora zaidi na hata wa kuhonga mahakimu, wana haki zaidi kuliko wale ambao hawana uwezo huo, umma wa wafanyikazi na mafukara wa dunia. Aidha, shughuli za mawakili hasa zinazowafanya kuwa mabepariuchwara zinahusu kutafsiri sheria kutoa huduma kwa mabepari kuhusu umilikaji na ulimbikizaji mali. Kweli, hakuna usawa wowote wa kisheria katika ubepari, labda kwa katiba tu ila siyo katika hali halisi ya maisha. Kama mwanamziki maarufu Remy Ongala alivyokuwa akikariri kwa nyimbo zake, ”mnyonge hana haki”.
Kwa maandishi, kwa maneno katika katiba za kibepari, kila raia ana uhuru wa kusoma, kuandika, kusambaza maoni yake, kujumuika na yoyote yule anayetaka, kuwa kwa mwanachama wa chama chochote kile cha kisiasa anachokichagua, kuchagua viongozi na kuchaguliwa kuwa kiongozi, kununua na kuuza hisa, kumiliki mali, na kadhalika. Bali hayo yanaishia kwa vitabu na makaratasi tu, na kwa propaganda za mabepari katika mikutano, redio, televisheni, katiba na magazeti, kwani katika ukweli halisi wa maisha ya kila siku mambo ni tofauti kabisa.
Ni wazi kuwa mabepari wenye mali wanatekeleza haki yao ya kusema zaidi kuliko wafanyikazi na mafukara. Kwani ili usikike ipasavyo lazima utangazwe na magazeti, redio na televisheni na wanaomiliki vyombo hivi vya mawasiliano ni mabepari. Kwa hivyo, kusema ukweli, vyombo vya habari vya nchi za kibepari vinasambaza siyo habari za watu wote wa nchi hizo bali habari za mabwanyenye, wenye mali. Habari tunazozipata na kuzitumia Kenya kutoka kwa magazeti, redio na televisheni za nchi ya Ulaya Magharibi na Marekani Kaskazini kwa kweli ni habari kutoka kwa macho ya tabaka la mabepari, wenye mali, ni propaganda za kueneza na kulinda mfumo wa ubepari na ukolonmamboleo. Ni muhali kupata habari kuhusu mapambano ya wafanyikazi huko Marekani Kaskazini, Japan ama Ulaya Magharibi, ama harakati za watu weusi za kujikomboa kutoka kwa ubaguzi wa rangi huko Marekani na Ulaya kwa kuwa habari hizo zinachujwa na kuchekechwa na mabepari wenye kumiliki vyombo vya kusambaza habari. Uhuru wa vyombo vya habari ni uhuru wa mabepari wa kutumia waandishi wa habari na watangazaji habari kueneza itikadi ya kibepari. Wenye kupinga ubepari ni muhali kupewa fursa ya kufanya hivyo kwenye vyombo vya habari vinavyomilikiwa na mabepari. Na katika nchi za kibepari mabepari ndiyo wenye ukiritimba wa vyombo vya habari.
Hali kadhalika, katika nchi za kibepari mtu ni pesa wala mtu si utu, unaheshimiwa na kutambuliwa siyo kutokana na uzalendo wako, vitendo vyako vya kiutu, elimu ama mawazo yako ya busara bali kutokana na kiasi cha pesa ulicho nacho. Hii ndiyo adili ya ubepari. Hivyo, mamilionea wanatangazwa na kusikilizwa zaidi kama viongozi wa nchi. Bali wale wanaopigania ukombozi wa kijamii, wanaosimamia masilahi ya wengi, mafukara na makabwela hawapewi fursa ya kusikilizwa na wengi. Nchini Kenya, kwa mfano, vyombo vya habari vinafanya kazi ya kuwakuza mabwanyenye na wahalifu wa kila aina hadi wakawa viongozi.
Mawazo ya Wakenya wanalazimishwa kuyakubali ni ati katika mataifa ya kibepari kila mtu ana fursa sawa ya kuchaguliwa kuwa kiongozi ni ya uongo wala hayana ukweli wowote katika hali halisi ya maisha ya kila siku. Kwanza kabisa dola za nchi za kibepari zinaongozwa na mabepari wenyewe. Haiwezekani hadi sasa kuwa Rais ama Waziri Mkuu huko Marekani Kaskazini, nchi za Ulaya Magharibi, Japan, Canada, Australia na New Zealand ikiwa wewe si milionea au ikiwa huungwi mkono na mamilionea. Aidha, mawaziri na wabunge wengi katika nchi za kibepari mara nyingi huwa ni mabepari ama mabeparimchwara na ni muhali kwa mfanyikazi ama maskini kuwa mbunge, sembuse rais. Kwani demokrasi ya kibepari inalengwa kulinda mfumo wa ubepari na masilahi ya mabepari na kwa hivyo kumewekwa vikwazo na vizingiti vya kila aina vya kuhakikisha kuwa inakuwa muhali kwa wanaotoka tabaka la wafanyikazi na wasiyo na mali kuchaguliwa kuwa viongozi.
Siasa za kibepari ni siasa za pesa na kampeni zimejaa hongo, ufisadi, udanganyifu na mbwembe za usonko na propaganda za kila aina za kuwarubuni wapigaji kura. Ikiwa huna hela basi huwezi kugharamia kampeni, huwezi kupata fursa ya kuwasiliana na wananchi unaowaomba wakupigie kura. Kwani ingawa kuna uhuru wa kujumuika na kushiriki kwa chama cha kisiasa unachokitaka ili kuwe na mikutano lazima kuwe na pahali pa kufanyika hiyo mikutano. Na majumba ya mikutano ni mali za matajiri. Kwa hivyo, mabepari wana uwezo zaidi wa kufanya mikutano kuliko wafanyikazi ama makabwela. Isitoshe, mara kwa mara vyombo vya dola vinatumika kupiga, kuzuia na kuparaganya vyama, migomo, mikutano, maandamano na juhudi zote za kujizatiti za wafanyikazi na viongozi wao za kupigania masilahi yao ya kitabaka.
Uhuru wa kuabudu ndiyo unaoungwa mkono sana na serikali za kibepari kwani kutoka zamani dini imetumika sana kueneza adili ya tabaka linalotawala katika jamii. Dini imetumika na inaendelea kutumika kuwakanganya umma wanaonyonywa na kugandamizwa kuvumilia na kukubali utumwa, ukabaila, ubepari, ukoloni na ukolonimamboleo. Kwa hivyo, mabepari wanatetea sana uhuru wa kuabudu kwa maneno na kwa vitendo. Ila wakati wote mabepari wanatetea dini zao wenyewe na kubagua dini zingine. Kwa mfano, huko Marekani Kaskazini na Ulaya Magharibi mabepari ambao wanajitambulisha na dini za Kikiristo na Kiyuda, wanatumia nguvu za dola na za kiuchumi kupiga vita baridi na moto Uislamu na dini zingine. Na huko Uingereza serikali inayoongozwa na Waprotestanti inawabagua sana Wakatoliki. Bali huu ndiyo unafiki wa uhuru wa kuabudu mabepari wanaojigamba nao. Kutokana na sera za kinafiki ambazo ni sehemu ya ubepari na ubeberu, dunia inakumbwa na tatizo kubwa, hatari kwa usalama na amani – tatizo nyeti la ugaidi.
Katiba za kibepari zinawahakikishia raia wote haki ya matibabu, haki ya kupata elimu bora, haki ya kuishi kwa nyumba bora, haki ya kuajiriwa kazi na kadhalika. Lakini katika hali halisi ya maisha wanaotekeleza haki hizi kama invyostahili ni mabepari, matajiri, wenye mali. Kwani wenye uwezo wa kipesa ndiyo wanaoweza kupata matibabu bora zaidi na kwa hivyo matajiri wanatekeleza haki ya kuwa na afya bora kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko wafanyikazi. Watoto wa matajiri wanapata elimu bora zaidi kuwaliko wa maskini na makabwela kwa kuwa ukiwa na fedha unaweza kuwapeleka wanao katika shule za binafsi za hali ya juu zaidi. Kuhusu nyumba, ni wazi kuwa kuna mamilioni ya watu katika nchi tajiri za kibepari ambao hawana makao kabisa, mamilioni wanaishi kwa mitaa ya mabanda huku maelfu wasiyo na makao wanalala katika vituo vya reli, mabasi na mabomba ya kupitisha takataka na vyoo. Mitaa ya mabanda ni sehemu ya maisha katika nchi za kibepari, hasa za nchi zilizoko chini ya ukoloni na ukolonimamboleo. Wakati huo huo wenye mali wanalala kwa makasri ya majumba. Wakati wengi hawana makao, kuna nyumba nyingi tupu zinazosubiri watu wenye uwezo wa kuzikodisha au kuzinunua. Ukosefu wa ajira na mishahara duni kwa wale wenye ajira ni sehemu ya mfumo wa ubepari na kwa hivyo idadi kubwa ya watu hawana uwezo wa kutekeleza haki ya kuwa na ajira iliyoko katika katiba za nchi za kibepari.
Haki ya kusafiri inatekelezwa zaidi na mabepari wenyewe, kwani ingawa kila raia ana haki ya kusafiri popote anapotaka katika nchi yake na ulimwenguni, wenye mali wanasafiri zaidi na mbali zaidi. Watalii wengi wanaozuru Kenya yetu kila siku kutoka Marekani Kaskazini na Ulaya Magharibi, kwa mfano, wengi wao ni mabepari, mabeparimchwara au waliyobahatika kuajiriwa kwa kazi zinazolipapa mishahara mikubwa na marupurupu manono. Ni wafanyikazi wachache mno kutoka nchi za kibepari wanaoweza kutalii Afrika.
Kwa muhtasari, tunasema kuwa demokrasi ya kibepari ambayo ilipambaniwa na mabepari na makabwela ikiwa ni pamoja na wajoli na wanamapinduzi iliwaletea binadamu uhuru zaidi kuliko hapo awali, lakini ni demokrasi ya wenye mali. Kwani mabepari ndiyo wanaochaguliwa kuongoza serikali katika nchi za kibepari, ndiyo wenye sauti, ndiyo wanaotunga sheria, ndiyo wanaotengeneza sera za ndani ya nchi na za mahusiano na nchi za kigeni. Kwa vyovyote vile wao ndiyo wenye haki zaidi kwa kuwa wao ndiyo wanaomiliki njia kuu za uzalishaji mali na hivyo uchumi na siasa. Kwani tumesema hapo awali kuwa matabaka mawili tofauti hayawezi kuwa na haki sawa wakati mmoja, tajiri na maskini kamwe hawawezi kuwa na demokrasi sawa.
Tutatoa mfano kufafanua jambo hili. Ukikodesha nyumba unakuwa mkodeshaji. Nyumba si yako, ni ya mwenye nyumba, bwanyenye. Na kwa sababu hii, huwezi kuipiga rangi unayoitaka hiyo nyumba. Wala huwezi kuamua kuifanyia marekebisho yoyote pasina idhini ya mwenye nyumba. Si wewe unayeamua kuhusu kodi ya nyumba itakuwa shilingi ngapi kila mwezi, bali ni mwenye nyumba. Mwenye nyumba anaweza kuifanyia hiyo nyumba unayoikodisha marekebisho yoyote anayotaka kwa kuwa ni yake. Hali kadhalika hahitaji idhini yako ndipo apandishe kodi ya kila juma, mwezi au mwaka. Fauka ya haya akikata shauri tu atakupa ilani utoke kwa nyumba hiyo hata kama wewe mwenyewe unapendelea kuendelea kukaa kwa nyumba hiyo. Sidhani kuna mkodeshaji wa nyumba ambaye atakanusha ukweli kuwa mkodeshaji hana uhuru au demokrasi kuhusu nyumba anayoikodesha, mwenye uhuru na demokrasi ni mwenye nyumba. Chambilecho Muamar Gadaffi, mtu mwenye mahitaji na anayetegemea mwingine kwa mahitaji yake, ni mtumwa kwelikweli.
Basi ndivyo ilivyo kwa kila hali, kila mara wenye demokrasi ni wale wanaomiliki ama kudhibiti njia kuu za uzalishaji. Anayetawala mahitaji yako na njia ya kujipatia riziki vilevile anakutawala, hakuna usawa wowote kati yako na yeye. Na kwa kuwa katika mfumo wa ubepari, mabepari ndiyo wanaomiliki njia kuu za uzalishaji wanatawala mahitaji ya wafanyikazi na makabwela, na kwa hivyo mabepari ndiyo tabaka tawala, ndiyo wenye demokrasi.
Pamoja na haya yote, ni muhimu kukariri kuwa demokrasi ya kibepari ni zao la mapambano makali na ya muda mrefu mno. Ililetwa na mapambano ya wajoli na mabepari na matabaka na makundi mbalimbali ya makabwela yaliyokuwa yakinyanyaswa na mfumo wa ukabaila na ufalme. Na kutoka iwasili, imekuwa ikijengwa na kuendelezwa na mapambano ya wafanyikazi yakiongozwa na wanamapinduzi. Yaani haki zote zile zilizoko katika ubepari leo hazikuweko siku zote. Zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku kutokana na mapambano ya wafanyikazi na umma ambayo yamekuwa yakiwalazimisha mabepari wakubali kufanya marekebisho ya kimaendeleo. Maelfu kwa maelfu ya wafanyikazi wamekufa katika uwanja wa mapambano ya kuupinga ubepari na mapambano ambayo yamefanya hali ya umma kuwa bora na bora zaidi.
Viwango vya demokrasi ya kibepari ni tofauti kati ya mataifa. Kwa mfano, katika nchi zinazotawalwa na siasa za usoshalisti wa kidemokrasi, kama Norway, Sweden, Finland na Denmark wafanyikazi wana haki zaidi za kidemokrasi na huduma bora na nyingi zaidi za kijamii kuliko katika nchi zingine zinazotawalwa na siasa za ubepari halisi kama USA, Wingereza, Ufaransa na Japan. Bali kwa vyovyote vile demokrasi ya kibepari ni ileile tu, demokrasi ya mabepari. Haki zote wafanyikazi walizo nazo ndani ya ubepari hazijabadilisha hali yao ya kuwa tabaka linalotawalwa, linalonyonywa, linalotumikia ubepari na mabepari. Isitoshe, vyama vya usoshalisti wa kidemokrasi Ulaya, mkiwemo nchi za Skandinavia, hivi leo vimekuwa vya kibepari kabisa. Serikali za kibepari na za ”usoshalisti wa kidemokrasi” zinazidi kuwanyang’anya wafanyikazi na makabwela wa nchi zao haki zote walizokuwa nazo hapo awali. Kutokana na utekelazaji wa sera za kibepari, ukosefu wa ajira na ufukara unazidi huku pengo kati ya matajiri na maskini likizidi kupanuka. Haki za maji masafi, lishe ya kutosha na bora, nyumba, nishati na huduma za kijamii mkiwemo afya, elimu, usafiri na usalama wa kijamii zinazidi kughalika na kunyang’anywa umma huku sera za kiuchumi za ubinafsishaji zikizidi kutekelezwa.
Pili, ni muhimu kutaja hapa kuwa kwa vyovyote vile demokrasi ya kibepari ni bora zaidi kuliko hali ilivyo katika nchi zilizoko chini ya ukoloni ama ukolonimamboleo. Watu wanatekeleza haki zao za kidemokrasi mara nyingi zaidi katika nchi za kibepari kuliko katika nchi nyingi za Afrika, Amerika Kusini na Asia zilizoko chini ya himaya ya dola zinazodhibitiwa na vibaraka wa mabeberu wanaotia fora kwa imla. Pengine hili linaweza kueleza kwa nini Wakenya wengi wanaopigania demokrasi na haki za binadamu wanatafuta kugeuza Kenya kuwa kama Amerika Kaskazini, nchi za Ulaya Magharibi, Japan, na kadhalika zenye demokrasi ya kibepari. Maana kwa kweli demokrasi ya kibepari ni bora mara nyingi kuliko imla iliyoko Kenya na nchi nyingi za Afrika.
Tatu, mabepari wanajigamba sana na demokrasi yao ya kibepari. Wanadai kuwa, ili nchi iwe ya kidemokrasi lazima iwe na demokrasi ya kibepari. Ati demokrasi iliyoko Amerika Kaskazini, nchi za Ulaya Magharibi, Japan, Australia, Canada na New Zealand ndiyo kilele cha demokrasi. Na hata wasomi wa kibwanyenye wanapojadili demokrasi mara kwa mara wanataka tufikirie kuwa demokrasi ya kibepari ndiyo ya hali ya juu zaidi na ya mwisho. Demokrasi yenyewe, kama vile ubepari, inazungumziwa kana kwamba haina historia, kana kwamba haikui na kuongezeka kutokana na kukua kwa nyenzo za uzalishaji nana harakati za kitabaka. Na hata wale wasabili wanaopiga hatua mbele na kuikosoa demokrasi ya kibepari, ukiwauliza suluhisho watakueleza kuhusu kurekebishwa kwa ubepari na demokrasi ya kibepari wala hawathubutu kujadili kuhusu demokrasi yoyote nyingine ya hali ya juu zaidi na iliyo nje ya mfumo wa ubepari. Lakini kama tutakavyoona, haya yote yana sababu zake. Mabepari hawataki kuuvunja mfumo wao wa ubepari, wala jukumu hilo la kuuvunjilia mbali mfumo huo na kuleta uhuru zaidi kwa jamii si jukumu lao. Ni jukumu la wanaonyonywa na kugandamizwa, ni jukumu la wafanyikazi na umma. Ni jukumu la wanamapinduzi. Jukumu la demokrasi ya kibepari ni kulinda na kuhifadhi mfumo waoubepari na ubeberu wa kupinga ukombozi na utkelezaji wa haki za binadamu za wengi.
9.3. Harakati za kitabaka
Tukirudi nyuma kidogo pahali tulipokuwa, tuliona kuwa kutoka mwanzoni mwa ubepari, wafanyikazi waligundua, kwa uchungu, ukweli tuliousema hadi sasa kuhusu demokrasi ya kibepari.
Hata hivyo, lazima tukumbuke na kusisitiza tena na tena kuwa maisha ya wajoli kama wafanyikazi chini ya ubepari yalikuwa bora zaidi na ya uhuru mara nyingi zaidi kuliko wakati wa ukabaila. Demokrasi hii ya ubepari iliwaongezea wajoli na makabwela uwezo wao wa kufurahia haki za binadamu kwa kiasi kikubwa zaidi kulingana na hapo awali.
Kwa mfano, sasa walikuwa wajoli na makabwela na hivyo walikuwa huru kuuza nguvukazi yao kwa bepari yoyote na pahali popote. Wangeweza kunyonywa na tajiri yoyote waliyolazimika kumfanyia kazi tofauti na wakati wa ukabaila ambapo walilazimika kumtumikia kabaila mmoja tu siku zote wapende wasipende. Walikuwa na uhuru zaidi wa kutembea na walianza kujishindia haki ya kupiga kura.
Tunakariri, mapambano ya wajoli na mabepari hatimaye yalileta hali ya leo ambapo kila raia wa nchi za kibepari ana uhuru wa kushiriki kwa chama chochote cha kisiasa anachokichagua na kuchagua serikali anayoitaka na wabunge anaowataka. Bali kama tulivyoona, siasa za kibepari zimejaa uhange, unafiki na ufisadi na pesa ndizo zinazoamua kila kitu. Hivyo, uhuru huu ni wa kuchagua ni chama gani cha kibepari kitawaongoza. Ni uhuru wa kuchagua ni mamilionea gani watakuwa kwa bunge, kongresi ama seneti Ni demokrasi ya kuamua kuhusu ni wanyonyaji gani watakuwa Marais ama Mawaziri Wakuu. Vyama vya mlengo wa kushoto vinavyopinga ubepari na ubeberu na vile vyote vinavyopigania masilahi ya wengi vimewekewa kila aina ya vikwazo kuvizuia kukua na kuenea. Vyombo vya habari, pesa na hata dola hutumiwa kupambana dhidi ya vyama vya kimapinduzi na kimaendeleo katika nchi za kibepari. Umma unaishi na propaganda kali za mabepari na mabeberu zenye lengo la kuwazuia kushiriki katika harakati za kupigania ukombozi wao. Ndiyo kwa maana hivi leo kila pahali katika nchi za kibepari idadi ya watu wanaojisajili kwa vyama vy kisiasa inapungua. Aidha, idadi ya wapigaji kura katika chaguzi za kitaifa inapungua kila mara.
Katika ubepari wajoli ambao sasa ni maprotetarii walikuwa na uhuru zaidi wa kukutana, kusema, kusoma, kuchapisha na kusambaza mawazo yao kuliko hapo awali. Hatimaye wafanyikazi walijinyakulia haki ya kuunda vyama vyao vya wafanyikazi vya kupigania masilahi yao ya kiuchumi kama wavujajasho. Hatutasita kusisitiza kuwa haki zote hizi hawakupewa kwa huruma za mabepari. Mabepari ni mabepari tu, hawana huruma yoyote kwa wafanyikazi, wanachofikiria kila mara ni kuzidisha mtaji wao na kuongeza faida tu basi. Haki walizokuwa nazo wafanyikazi hazikuanguka kutoka mbiguni wala hazikuletwa na maombi; katiba zilizowahakikishia haki makabwela hazikuteremshwa kutoka ahera jinsi Korani Tukufu ilivyoteremshwa wala hazikupatikana kwa mara moja kufumba na kufumbua na kwa msitari ulionyoka.
Kila hatua wafanyikazi na wote wanaonyanyaswa wamepiga mbele kuelekea kwa uhuru zaidi na kwa kuongeza kutekelezwa kwa haki zao za binadamu, imetokana na muungano na mshikamano wao wa mapambano makali na ya muda mrefu ambayo yamedai wengi kujitolea mhanga. Kwa muhtasari, tunaweza kutilia manani ukweli halisi kuwa demokrasi na haki zote za binadamu zinazofurahiwa na watu katika nchi za kibepari, zimetokana na juhudi za mapambano ya ukombozi ya wafanyikazi, wapenda maendeleo, wanamapinduzi na umma unaogandamizwa. Hii ndiyo maana ya harakati za kitabaka ambazo ndizo huzungusha mbele gurudumu la mageuzi na maendeleo, gurudumu la kimapinduzi linalozunguka mbele kumkomboa mfanyikazi na kila binadamu kwa ujumla kutoka kwa mfumo katili wa ubepari ambao sasa unapinga uhuru na ukombozi wa jamii.
9.4. Makinzano ya ubepari na chimbuko cha ubeberu
Kwa muda mfupi tu, miongo michache, ubepari uliongeza nyenzo za uzalishaji kwa wingi na ubora mara nyingi zaidi kuliko wakati wa mfumo wa ukabaila uliodumu kwa maelfu ya miaka. Kweli ubepari ulifungua mfereji wa uhuru, uvumbuzi, maendeleo na mapinduzi ya kitamaduni, kisayansi na kitekinolojia uliyokuwa umefungwa na mifumo ya utumwa na ukabaila kwa miaka na mikaka. Kwani baada ya kuingia kwa ubepari katika karne ya kumi na tisa, sayansi na tekinolojia ilipiga hatua nyingi mno mbele, na kuongeza uzalishaji mara nyingi zaidi, vyombo vipya tilatila viligunduliwa, mashini za kila namna zikajitokeza, bidhaa ambazo hazikuwahi kutengenezwa zikaonekana viwandani na sokoni.
Kwa maneno mengine, uhuru wa jamii na uwezo wa binadamu wa kutekeleza haki za binadamu za kula, kusafiri, kuwa na afya bora na kuishi muda mrefu iwezekanavyo, kuwa na nyumba bora, kuvaa nguo bora zaidi, kusema, kupunguza muda wa kufanya kazi na kupata muda wa kujielimisha na kujiburudisha, uliongezeka sana kwa wingi na ubora katika mfumo wa ubepari, kwani hatua zilipigwa mbele na kwa haraka sana kila siku za kuvumbua na kuendeleza kilimo cha mimea na ufugaji, madawa na matibabu, barabara na reli, magari, matreni, meli, ndege, matrakta na mitambo ya aina nyingi. Majumba yakajengwa kwa wingi, viwanda vikaota kama uyoga, na miji mikubwa ikakua na kupanuka na watu wengi zaidi wakaajiriwa mijini. Kwa upande wa utamaduni, wasanii wa nyanja za fasihi, muziki, uchoraji, ufinyanzi, maonyesho, falsafa wakajitokeza kwa wingi zaidi. Mawazo mapya yakajitokeza kuusaili na kuupiga vita utamaduni wa kishenzi, ushirikina na wa kupinga maendeleo. Sayansi ya uchumi na sayansi ya kimaumbile, biolojia, fizikia, kemia, jiolojia, jiografia na isabati ikazidi kusonga mbele kuzigundua, kuzielewa na kuzitawala sheria za kimaumbile kwa ajili ya kuongeza uhuru wa binadamu.
Kwa muhtasari, kwa muda mfupi kulingana na mifumo ya hapo awali katika historia ya binadamu, ubepari ulileta utamaduni na ustaarabu wa hali ya juu ambao haukuwahi kutokea hapo awali. Yaani uhuru wa binadamu katika mfumo wa ubepari ulikua kwa kasi mara nyingi zaidi kuliko ulivyokua katika mifumo ya utumwa na ukabaila. Na sababu moja ni kuwa ubepari ulivurugavuruga na kuvunjavunja mawazo yote ya ushirikina (kama ya dini) na kukiuka mila na miko ambazo zilitumika kwa maelfu ya miaka kupinga maendeleo ya binadamu. Binadamu nje ya dini, ushirikina na miko za kupinga mageuzi, akawa huru zaidi kufikiri, kuvumbua na kufanya utafiti wa kisayansi na kusambaza mawazo yake ya kimaendeleo.
Mabepari na wasomi wa kibwanyenye walipiga vita chochote kile kilichokuwa kikwazo kwa kukua kwa mtaji, kupanuka kwa masoko na kuongezeka kwa utajiri wao. Kwani mabepari hawakuwa (na hawana hata leo) taifa, dini, rangi, huruma, mipaka, miungu ama adili yoyote ile wanayoizingatia kwa dhati isipokuwa faida, pesa. Mungu na adili ya mabepari – licha ya madai yao yote ya Ukiristo, Uislamu, Uhindu na imani zingine – ni ziada, ni mtaji.
Kama tulivyosema, waliokuwa na haki ya kufurahia matunda ya utamaduni na ustaarabu huu walikuwa mabepari, matajiri, waajiri, wenye kumiliki na kudhibiti uchumi wa biashara na viwanda. Waliyokuwa wanafaidi zaidi (na wanafaidi hata sasa) kwa maendeleo ya sayansi na tekinolojia katika ubepari ni mabepari tu kwa kuwa ndiyo wanaoitumia kuongeza uzalishaji mali katika viwanda vyao na kwa hivyo kuzidisha utajiri wao. Kwani kwa wafanyikazi na makabwela, maendeleo ya sayansi na tekinolojia yanazidisha huzuni, ufukara na umaskini kwa kuwa yanaongeza kunyonywa kwao na ukosefu wa kazi miongoni mwao.
Kukua kwa nyenzo za uzalishaji na mashindano baina ya mabepari na mabepari yakawa yanazidisha mtaji na utajiri kwa watu binafsi ama makundi ya watu binafsi ya mabepari. Kilichokuwa kinazalishwa na jamii kikawa kinanyakuliwa na watu binafsi. Isitoshe, makampuni makubwa yakawa yanapanuka na kumeza yale madogo, viwanda vidogo vikamezwa na vikubwa na hivyo utajiri wote wa jamii ukawa unahodhiwa na mabepari wachache. Yaani, watu wachache wakaweza kukusanya mamilioni na mabilioni ya pesa, mtaji, mikononi mwao. Mtaji wa pesa ukazidi kupanuka na kukua na kutawala jamii zaidi kuliko ule wa viwanda na biashara.
Sasa kutokana na kukua kwa nyenzo za uzalishaji na kutokana na hali ya umaskini na ufukara ya wafanyikazi, ubepari katika kiwango hiki ulizalisha bidhaa nyingi tilatila ambazo sasa zilikosa soko ya kutosha nyumbani, wakalazimika kulimbikiza thamani ya mabilioni ya mtaji katika maghala. Ikaanza kuonekana wazi kuwa ubepari hauwezi kupanuka zaidi kuliko kiwango hiki cha ubeparihodhi huko Wingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ubelegiji, Japan na kadhalika. Mtaji haungeweza kuendelea kujizalisha na kujiongeza zaidi kwa kuwa bidhaa zilizokuwa zinazalishwa hazikuwa zinanunuliwa maana idadi kubwa zaidi ya wananchi wa nchi za kibepari walikuwa mafukara. Bidhaa zilikuwa zinakosa soko na kurundikana katika maghala. Katika kiwango hiki cha uchumi wa kibepari unaotawalwa na sheria ya utashi na ugamvi, ugamvi ulizidi utashi na kwa hivyo kimantiki ikawa ni hasara na kujifilisi kuendelea kuzalisha zaidi.
Wakati huo huo viwanda vya mabepari vilihitaji sana malighafi ambayo ama ilikuwa haba ama haingeweza kupatikana kabisa nyumbani. Hali kadhalika wafanyikazi walizidisha mapambano yao. Migomo na maandamano ya mara kwa mara ya kudai nyongeza za mishahara, kupunguzwa kwa masaa ya kufanya kazi, hali bora kwa wafanyikazi kazini, na kadhalika, yakawa yanawalazimisha mabepari kuwaongeza ujira, kuwapunguzia masaa ya kufanya kazi, kuwalipwa ovataimu, kuongeza marupurupu, kurekebisha mazingira ya kufanyia kazi na kwa ufupi kufanya maisha ya wafanyikazi kuwa bora na bora zaidi ingawa bado katika hali ya unyonyaji. Lakini haya yote yalisaidia kupunguza faida ya mabepari. Gharama zikazidi kuongezeka siku hadi siku na kuzidi kupunguza mtaji wa mabepari. Mashindano kati ya mabepari yakaleta ukiritimba juu ya masoko huria na hatimaye mtikisiko wa uchumi na fedha wa mara kwa mara ndani ya nchi za kibepari.
Tumesema kuwa kila mara mabepari ni watu wanaoabudu mungu wa faida, pesa, utajiri, mali, ziada, mtaji. Kwa sababu hii, haiwezi kuyumkinika kuwa mabepari wangewahurumia wafanyikazi na wachochole, kwa moyo wa uzalendo na ubinadamu na kutumia mabilioni ya pesa na mali walizozilimbikiza benki na mtaji kwa maghala kwa ajili ya huduma kwa wafanyikazi na kwa jamii ya nchi zao! La, hasha, mabepari kamwe hawawezi na hawajaweza kufanya hivyo popote ulimwenguni. Kwani ubepari ni unyama.
10. Ubeberu
10.1. Ubeberu
Kwa hivyo, mabepari wakawa wanatafuta suhulisho la kuendelea kuchuma faida na kuongeza mtaji wao. Na hatimaye wakapata suhulisho hilo: kusafirisha mtaji wa ziada kutoka Wingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ubelegiji, Ulaya Magharibi na Japan hadi Afrika, Asia na Amerika Kusini. Kwani katika nchi hizi kulikuwa na nguvukazi ya kunyonya kwa urahisi, hata ya shokoa. Vilevile, kulikuwa na uwezo wa kupata soko kwa bidhaa zao zilizokuwa zikioza kwa maghala. Aidha, kulikuwa na malighafi tele ambayo wangepora kwa wingi na kwa urahisi. Hivyo, wakaona njia ya kujiongezea faida na kupanua mtaji wao tena, sehemu kidogo ya ziada ambayo wangeipata kutoka kwa kupora na kunyonya sana mali na watu wa makoninenti ya Afrika, Asia, Amerika na Karibiani, wataitumia kuwatupia hawa wafanyikazi matata wa nyumbani ili angalawa kupoza ama kupunguza harakati za kitabaka.
Hii ndiyo mantiki ya ubeberu, hivyo ndivyo ubeberu ulivyokua kutoka kwa ubepari na ukavamia Afrika, Asia na Amerika Kusini kama ukolonimkongwe na leo ukolonimamboleo. Hali hii ndiyo iliyoleta kile ambacho kimekuja kujulikana kama kinyang’anyiro cha Afrika ambapo mabeberu walipigania na kushindania kubakua sehemu za Afrika ili kuzifanya makoloni yao. Hatimaye wakafanya kongamano huko Berlin, Ujerumani, mnamo mwaka wa 1888 ambapo bila hata kuwahusisha Waafrika, waligawanya Afrika na kuifanya makoloni ya nchi za kibeberu za Ulaya Magharibi.
10.2. Ukolonimkongwe
Ukolonimkongwe ni kiwango cha kwanza cha ubeberu, ambapo ubeberu wenyewe ni kiwango cha juu zaidi cha ubepari. Ukolonimkongwe haukuja kwa lengo lingine lolote nchini, Afrika na popote duniani isipokuwa kunyonya na kupora rasilmali na maliasili. Ukolonimkongwe ulichukua nafasi ya ukabaila wa Ulaya ambao tayari ulikuwa umenyonya na kupora Afrika, India, Amerika Kaskazini na Kusini na kadhalika kwa miaka mingi kutokana kwa biashara ya upunjaji ya viungo vya kukokeza mlo, dhahabu, watumwa na bidhaa zingine. Afrika iliumizwa mno na biashara hiyo hasa biashara ya watumwa. Kweli, biashara ya watumwa ilirudisha Afrika nyuma sana kwa kila hali. Biashara ya watumwa ambayo yenyewe ni uvunjaji wa haki za binadamu usiyo na kifani, ilivuruga, iliparaganya na kuzuia maendeleo ya uhuru wa Wafrika. Ilikuwa kikwazo cha kukua kwa uwezo wa kutekeleza haki za binadamu.
Ukolonimkongwe wa Wingereza ulituvamia kutunyonya, kutunyanyasa, kutupora na kutugandamiza kama taifa na kama watu Weusi kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kwa kila hali. Wakoloni walileta dola lao Kenya ambalo lilikuwa chombo cha wakoloni, walowezi na watu weupe cha kuendeleza na kudumisha mahusiano ya kikoloni ya kutudhulumu wenyeji katika nchi yetu wenyewe. Kweli wakoloni walitumia visingizio vingi kuhalalisha utawala wao wa kidhalimu. Walidai ati wamisheni wa dini mbalimbali walikuja kutekeleza jukumu lao la kikiristo la kutukokota na kututoa kutoka dini, imani na mila za giza na kifo, ati kutoka kwa ushirikina na desturi za kishenzi na kutuonyesha dini ya ukweli ya Ukiristo. Ati walivamia nchi yetu kutuweka katika barabara sahihi na ya mwangaza wa uzima wa milele.
Wamisheni walitumiwa na mabepari wa nchi yao kutupiga vita vya kisaikolojia, kutufanya tujidharau sisi wenyewe, tulaani miungu ya mabibi na mababu zetu, tukane historia yetu na utamaduni wetu, tufikirie kuwa daima watu Weupe ni watu zaidi kutuliko sisi watu Weusi. Badala ya utamaduni wetu wa jadi uliyotupa kujiamini na kujitegemea kwa kila hali, tukapachikwa utamaduni wa kutegemea watu wengine, mabeberu, kutatua matatizo yetu. Badala ya usanii na ubunifu tukatumbukizwa katika barabara ya ukasuku na kutegemea bahati na majaliwa ya maumbile na Mwenyezi Mungu. Wamisheni kwa kutumia njia mbalimbali wakalenga kuuhalalisha ukoloni nchini kwa kueneza propaganda kuwa ukoloni wa Wingereza Kenya ulikuja kutusaidia, kutustaarabisha, kutuelimisha na kutupeleka katika barabara ya uhuru, maendeleo na ustaarabu.
Hata hivyo, ni muhimu tusisitize hapa kuwa tangu utuvamie mnamo mwaka wa 1888, watu wetu hawakuukaribisha ukoloni. Waliupinga kwa kila hali. Wakenya walitetea haki yao ya kujitawala na kujiamulia sudi yao wenyewe kila mara na kwa njia mbalimbali. Walipigania kujihami na kulinda heshima ya mtu mweusi. Walipigana kufa na kupona kwa kutumia njia mbalimbali mkiwemo mapambano ya silaha. Lakini kutokana na sababu kuwa wakoloni waliyotuvamia walikuwa na silaha bora kutuliko na kwa sababu wakati huo hatukuwa taifa, kila kabila na koo ilipigana dhidi ya ukoloni kivyake bila kusaidiwa na kabila au koo lingine, wakoloni walitushinda na wakafaulu kufanya Kenya kuwa koloni yao mnamo mwaka wa 1920. Ukoloni uliyotuvamia ulikuwa sehemu ya ubepari ambao ulikuwa mfumo wa hali ya juu zaidi kufungamana na nyenzo za uzalishaji kuliko mfumo wa umajumuiuliyokomaa wa makabila mengi ya Kenya wakati huo. Kwa maneno mengine, watu wa Wingereza walikuwa huru zaidi kutuliko na wakatumia uhuru wao kutuvamia na kututawala katika nchi yetu wenyewe. Bali kwa Kenya kufanywa kuwa koloni la Uingereza hakukuwa na maana kuwa Wakenya waliinua mikono na kuwacha kupigania uhuru wao na haki yao ya kujitawala na kujiamulia sudi yao kama taifa.
Tumeona kuwa kabla ya kuja kwa ukoloni makabila mengi ya Kenya yalikuwa yamefika kiwango cha juu sana na cha mwisho cha mfumo wa umajumuia, umajumuiuliyokomaa. Tulikuwa tunapiga hatua mbele kimaendeleo wala hatukuwa tumekwama. Kila siku tulikuwa tunasonga mbele kwa kilimo, kwa uvumbuzi, kwa sayansi na tekinolojia, kwa ujenzi na kwa sanaa. Nyenzo za uzalishaji zilituwezesha kuwa na utamaduni uliyokuwa unatosheleza mahitaji yetu katika hali halisi ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Tumeona kuwa wenzetu katika ufuo wa bahari, Waswahili, walikuwa wameendelea sana na hata walikuwa katika kiwango cha mwanzo cha mfumo wa ukabaila. Ukoloni ulipotuvamia ulipiga utamaduni wetu vita na kuhakikisha kuwa hatuendelei bali tunakwama kisiasa, kiuchumi, kisayansi na kitekinolojia na kwa kila hali. Aidha, wakoloni walipambana vikali dhidi ya historia yetu wakiwa na nia ya kuvunjavunja chochote kile tulichokuwa tumekifanya na kutuwacha katika hali ya kutojiamini, kujidharau na kufikiria kuwa hatukuwa na historia thabiti nyuma yetu.
Ukoloni ukavurugavuruga mahusiano ya uzalishaji ya kiujima tuliyokuwa nayo na kutupachika mahusiano mapya na mageni ya kibepari. Ili watutawale na kutunyonya, iliwapasa wafanye hivyo. Haya waliyatekeleza kwa kuhakikisha wametupora njia kuu ya uzalishaji, ardhi, tuliyokuwa nayo na huku pia wakiharibu nyenzo za uzalishaji zilizokuwa sehemu ya utamaduni wetu wakati huo. Walowezi wakatunyang’anya mashamba hata mifugo yetu. Wakaanza kutulazimisha kulipa kodi za aina mbalimbali. Wakatumia kila mbinu kutushurutisha tuajiriwe katika mashamba ya walowezi wao waliyokuwa wametupora na ambayo yalikuwa mali ya watu wa Kenya. Tukaingizwa katika utamaduni wa kuzalisha siyo kwa ajili ya kutosheleza mahitaji yetu, bali kwa ajili ya kutajirisha wanyonyaji, walowezi.
Ukolonimkongwe vilevile ulikuwa ni mfumo wa ubaguzi wa rangi. Chini ya himaya ya ukoloni tuliporwa haki ya kutekeleza haki zetu za binadamu kama taifa. Tulikuwa tunatawalwa na kugandamizwa na watu weupe katika nchi yetu wenyewe. Tulidhalilishwa, kutukanwa na kubaguliwa na Wazungu kwa kila hali katika nchi yetu ya kuzaliwa. Hatukuwa na uhuru wala hatukuwa tunatekeleza haki za kidemokrasi chini ya katiba ya wakoloni. Tulilazimika kutii sheria dhalimu zilizokusudia kutushurutisha tukubali ukoloni na ambazo hatukushirikishwa kuzitunga. Jela zikajengwa kwa ajili ya kufunga Wakenya na polisi wa kikoloni wakatumiwa kujenga utamaduni wa kigaidi na kinyama dhidi ya Wafrika ambao walikuwa wanapachikwa woga, hofu na kimya mbele ya watu weupe. Tukafukarishwa na kufanywa watumishi wa Wazungu ndani ya nchi yetu wenyewe. Ikatupasa kuwatetemekea na kuwanyenyekea watu weupe na kuwa kama watumwa wao wa kuwazalishia, kuwalisha, kuwastarehesha na kuwatumikia kwa kila hali. Sisi watu weusi katika nchi yetu wenyewe tulihesabiwa kama watu wa mwisho, wa kwanza wakiwa Wazungu, halafu Wahindi, halafu Waarabu, halafu Wasomali (kana kwamba Wasomali si watu weusi!) na kishamwisho sisi weusi! Hatukuwa na demokrasi ama uhuru wa kuwa na uhusiano wowote ule na mataifa mengine ya ulimwengu. Kila kitu kuhusu maisha yetu kiliamuliwa na wageni, Waingereza, bila sisi kuhusishwa.
Ukolonimkongwe ulitumia dola, dini, ubaguzi wa rangi na propaganda dhidi ya watu weusi, ili kututawala, kutunyonya, kutunyanyasa na kutupora uwezo wa kutekeleza haki zetu za binadamu. Ndiyo kwa maana, mababu zetu hawakuchoka hata kwa dakika moja kupambana dhidi ya ukoloni na kugomea unyama wote uliyokuwa unatendewa wananchi wa Kenya na walowezi na serikali yao. Walitumia kila mbinu na hila kupigania uhuru na ukombozi wa taifa letu.
Kati ya mwaka wa 1920 na 1950, wazalendo wa nchi yetu waliongoza umma wa Wakenya katika harakati za kupigania ukombozi wa taifa letu kwa kutumia njia za kikatiba. Wakenya wakatumia mbinu za amani za kutumia katiba ya mkoloni kudai haki yao ya kuwa huru. Wafanyikazi na wakulima waliandaa migomo na maandamano mijini na mashambani. Wazalendo wa Kenya waliandika barua kwa wakoloni wakidai uhuru. Wakatuma wajumbe Wingereza kupeleka malalamiko ya Wakenya kwa wakuu wa serikali ya Wingereza moja kwa moja kutoka huko. Wakawa wanapigania haki ya kuunda vyama vya wafanyikazi na vya kisiasa chini ya ukoloni.
Hata hivyo, wakoloni wakawa hawasikilizi lugha ya amani ya Wakenya ya kudai uhuru wao. Wakawa wanauma mikono ya amani na badala yake wakazidisha utawala wao wa kikatili na kimabavu. Wakazidi kuwasaka, kuwakamata, kuwafunga na kuwaua wazalendo na wananchi waliyokuwa wakidai uhuru kwa kutumia njia za sheria ya mkoloni mwenyewe.
Kutokana na haya yote baada ya vita vya pili vya dunia Wakenya wakawa hawana budi ila kuanza kujizatiti kupigania uhuru wetu na haki za binadamu kwa kutumia silaha. Mnamo mwaka wa 1952 Wakenya wakatangaza vita vya ukombozi wa kitaifa. Vita hivi ambavyo vilisababisha maelfu ya Wakenya kufungwa, kuwekwa vizuizini, kuteswa, kuuawa na kufanyiwa unyama usiyo na kifani na wakoloni, hatimaye viliukwamua ukolonimkongwe nchini. Bendera ya mtu mweusi Kenya ikapandishwa mnamo mwaka wa 1963 na ile ya ukoloni ikashushwa. Historia ya vita vya kigorila vya Jeshi la Uhuru na Mashamba, maarufu kwa jina Mau Mau, daima ni kielelezo kuwa watu wakijaribu mbinu zote za amani za kupigania uhuru na ukombozi bali zikashindwa kuwakomboa, watakuwa hawana budi ila kujizatiti kwa vita na kupigania uhuru kwa kutumia silaha. Kwani vita vya ukombozi ni muundo wa hali ya juu zaidi wa mapambano ya kutatua makinzano katika jamii, kati ya mataifa, kati ya matabaka na baina ya makundi mbalimbali ya kisiasa yanayokinzana. Aidha, vita vya kupigania uhuru na ukombozi wa kijamii na kitaifa ni vita halali na vya kimaendeleo.
10.2. Ukolonimamboleo
Tumeeleza hapo awali kwamba historia ya binadamu, kama ile ya uhuru na utekelezaji wa haki za binadamu, husonga mbele daima. Lakini mwendo wa haki za binadamu siyo wa msitari uliyonyoka bali ni mwendo wa upogoupogo na uliyo na makinzano. Msingi wa historia ni maisha na msingi wa maisha ni maumbile. Na mwendo ni hali ya maumbile, bila mwendo hakuna maumbile na bila maumbile hakuna mwendo. Kila mara mwendo huleta hali mpya inayotarajiwa na isiyotarajiwa.
Turudi kwa mada yetu tukikumbuka haya. Kama tulivyosema hapo awali wakoloni hawakuwa na nia nzuri wakati walipovamia na kutawala nchi yetu. Hawakuvamia na kutawala nchi yetu kwa madhumuni ya kutustarabisha kama walivyokuwa wakidai. Wala hawakutawala nchi yetu kwa hiari yetu bali kwa mabavu. Pamoja na haya yote, ukoloni siyo tu ulivuruga mkondo wa maendeleo ya makabila ya nchi yetu bali pia wakati huohuo bila kukusudia kufanya hivyo ukoloni uliongeza uhuru nchini na hivyo uwezo wa utekelezaji wa haki za binadamu.
Kabla ya ukoloni hapakuwa na taifa la Kenya. Kulikuwa kunaishi koo na mbari za makabila mbalimbali nchini. Ni katika pwani ya Kenya, Mombasa, Lamu, Pate na Malindi ambapo kulikuwa na hisia za utaifa. Kulianza kuwa na taifa la Kenya wakati nchi yetu ilipofanywa koloni ya Wingereza mwaka wa 1920. Wakoloni ndiyo waliyounganisha makabila mbalimbali ya Wakenya na kuyaweka chini ya himaya ya ufalme wa Wingereza. Mipaka ya Kenya iliamuliwa na wakoloni katika Kongamano la kugawanya Afrika kati ya wakoloni wa Ulaya lililofanyika Berlin, Ujerumani, mnamo mwaka wa 1888. Kuanzia hapo ndipo ramani ya taifa la Kenya ikachorwa.
Isipokuwa tu katika mataifa ya kikabaila huko pwani, hapakuwa na dola nchini kabla ya kuja kwa ukoloni. Dola ni mashini ya tabaka moja ya kugandamiza tabaka lingine. Katika kutekeleza kazi yake ya ugandamizaji, mashini hii inayoitwa dola, hutumia vyombo vyake vya kuhofisha, kushawishi, kushurutisha na kunyanyasa. Vyombo hivi ni pamoja na sheria, polisi, magereza, majeshi, mahakama na serikali. Tumeona kuwa kabla ya ukoloni makabila ya Kenya katika bara ya nchi yetu yalikuwa katika kiwango kiwango kimoja ama kingine cha mfumo wa umajumuiuliyokomaa. Katika mfumo wa umajumuiuliyokomaa, bado jamii haikuwa na tabaka lililokuwa likitawala, kunyonya na kunyanyasa tabaka lingine. Kwa sababu hii hapakuwa na haja ya vyombo vya dola vya kulazimisha tabaka moja kukubali utawala wa tabaka lingine. Jamii ya mfumo wa umajumuiuliyokomaa iliishi kwa usawa ambao ulilindwa na adili, miko na mila ambazo zilikubaliwa na kila mtu katika jamii hiyo, basi hapakuwa na haja ya sheria wala mahakama ya kuhukumu wale ambao walikataa kufuata sheria. Wala hapakuwa na polisi ama magereza ama majeshi ya kutekeleza sheria na hukumu za mahakimu. Hapakuwa na haja ya ma-PC, ma-DC, ma-DO, machifu na masabuchifu wa kutawala watu wengine na kuwashurutisha kufanya mambo fulani. Haya yote yaliletwa na ukoloni. Waingereza walifanya Kenya koloni yao kwa mabavu.
Mwandawiro Mghanga,
Mwenyekiti wa Communist Party of Kenya (CPK)