Ijumaa hii, Machu 8 2019 ni Siku Kuu ya Wanawake Ulimwenguni. CPK tunaungana na wanawake wa Kenya kukumbuka na kusherehekea siku kuu hii pamoja na wakereketwa wa usawa wa kijinsia kote ulimwenguni. Wanawake nchini bado wanapigania haki za wanawake za kumiliki maliasili, mali na urithi wa wazazi wao sawa na wanaume. Huku wakizingatia hali za wanawake nchini, wanawake wanapinga siasa, tamaduni, maadili, mifumo na chochote kile kinachowabagua, kuwadhalilisha, kuwanyanyasa na kuwasukuma pembeni wanawake katika jamii ya Kenya. CPK daima tuko pamoja na wanawake na wanaharakati wa usawa wa kijinsia katika mapambano haya ya kuondoa mfumo wa udhalimu wa mtu kwa mtu.
Waanzilishi wa ukommunist wa kisayansi, Karl Marx na Fredrick Engels, waliwahi kuandika kuwa tunaweza kupima kiwango cha uhuru wa jamii fulani finyu kutokana na kiwango cha uhuru wa wanawake. Kadiri wanawake katika jamii wanavyokuwa huru zaidi ndivyo jamii hiyo, sawia, inavyokuwa huru zaidi. Nayo jamii inayozuia uhuru na ukombozi wa wanawake vilevile inapinga uhuru na ukombzi wa jamii yote kwa ujumla. Hivyo basi, harakati za ukombozi wa jamii kutoka kwa mifumo ya unyonyaji wa mtu kwa mtu lazima ziende sambamba na harakati za ukombozi wa wanawake na usawa wa kijinsia.
Katiba ya Kenya ambayo imetokana na mapambano makali ya umma wa Kenya ni hatua kubwa sana mbele ya kuelekea kwa demokrasi, uhuru wa kijamii na kitaifa, usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake. Changamato linalosalia kwa mkabala huu ni kuitafsiri na kuitekeleza katiba yenyewe ili isibaki ahadi za maneno matupu bali iwe vitendo halisi vya kuboresha maisha ya kila mtu katika jamii mkiwemo kuhakikisha usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Ndiyo kwa maana CPK tunalaani vitendo vya bunge za Kenya za kuvunja katiba ya Kenya kwa kukataa kutengeneza sheria ya kupiga hatua ya kutekeleza usawa wa kijinsia katika uwakilishaji bungeni. Wabunge wanawake waliyo katika msitari wa mbele wa kupigania uswa wa kijinsia bungen na taasisi zingine za uwakilishiji wa umma wanapaswa kuwa na ujasiri wa kuvihama vyama vya kisiasa vinavyozingatia mfumo wa ubepari na kuungana nasi kupigania ukombozi wa jamii kutoka kwa kila aina ya unyonyaji na unyanyasaji wa mtu kwa mtu. Vyama vya kisiasa vinavyotawala bungeni leo ni vya itikadi ya kibepari na ni muhali kuvitegemea kupigania ukombozi wa wanaodhulumiwa Kenya, mkiwemo wanawaki katika jamii.
CPK tunatambua kuwa kukiwa na usawa kati ya wanaume na wanawake katika jamaa, jamii na taifa, vilevile amani, haki na maendeleo yatakua kwa haki, usawa na kasi zaidi. Mwanamume anayemnyanyasa na kumnyima mke wake fursa ya kushiriki kikamilifu katika mipango ya jamaa yao ikiwa ni pamoja na uzalishaji, kumiliki pamoja ardhi, maliasili na rasilimali za jamaa, huzuia maendeleo ya jamaa yake sawia. Mwanamke akishirikishwa ipasavyo na mume wake katika uzalishaji na ugamvi wa kile kinachozalishwa, na katika usimamizi wa rasilimali, familia hiyo itaona manufaa makubwa na ya haraka. Maana mara nyingi wanawake ni wasimamizi na wahifadhi bora zaidi wa rasilimali za jamaa na jamii kuwaliko wanaume. Aghalabu, kwa mfano, mwanamke akipokea pesa za mazao ya shamba kama maziwa, kahawa, chai, mboga ,parachichi, makadamia, mboga na bidhaa zingine za kilimo, huzitumia kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani kwake ambayo hufaidi watoto na vilevile mume na mke. Kinyumeche, kuna visa vingi ambapo wanaume wanafuja pesa zinazotakana na juhudi za jamaa zao kwa anasa na starehe ambazo pia zinahatarisha jamaa nzima kwa maambukizo ya maradhi ya ulevi na ngono. Aidha, kuna taarifa ya visa vingi ambapo mume anafilisi jamaa yake kabisa kwa kuuza na kuponda mali na ardhi ya jamaa.
Usawa wa kijinsia ni haki ya binadamu. Maana binadamu wote ni sawa kwa mujibu wa kuwa binadamu, wawe wanawake wawe wanaume. Kwa wanaume kuwanyanyasa wanawake ni kutokuwa na shukrani kwa mama zetu ambao wametubeba miezi tisa tumboni mwao tena wakatuonyesha mapenzi kwa kutulea kutoka watoto hadi tukakua watu wazima. Isitoshe, kukubali hali ya kubaguliwa kwa wanawake katika jamii ni kushiriki katika kudhulumiwa kwa wasichana wetu tuliyowazaa, na pia dada zetu tuliyozaliwa tumbo moja. Ndiyo kwa maana, mzazi mzuri ni yule anayehakikisha usawa wa kijinsia nyumbani kwake; anayewafundisha watoto wake kutokana na mfano halisi wa uhusiano wake na mke wake kwamba wavulana na wasishana ni sawa na wanapaswa kukua wakizingatia ukweli huu kwa maneno na vitendo.
Nayo jamii lazima iendelee kupambana kuhakikisha kuwa wanawake wanajishindia uwezo wa kuwa na fursa sawa na wanaume kwa kila hali. Tena ikumbukwe kwamba harakati za ukombozi wa wanawake si za kuwafanya wanawake kuwa na uwezo wa kuwanyonya na kuwanyanyasa wanaume, si kuwawezesha wanawake kushiriki katika maovu yote yanayofanywa na wanaume leo. Harakati za kweli za ukombozi wa wanawake ni za kukomboa jamii kutoka kwa mfumo wa unyonyaji na unyanyasaji wa mtu kwa mtu. Ni za kukomboa jamii kutoka kwa mifumo ya kikatili na ya kupinga maendeleo kama utumwa, ukabaila, ubepari, ukoloni na ukolonimamboleo. Ni harakati za kuleta usawa wa kijinsia ambapo wanawake na wanaume wanashirikiana kwa haki, usawa, amani na mapenzi ya kweli. Ni kugawanya majukumu ya kijamaa na kijamii kwa ajili ya faida ya wote huku wakitambua tofauti zao za kimaumbile.
Tunakariri, hapawezi kuwa na maendeleo endelevu katika hali ambapo wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya watu wote nchini wananyanyaswa, wanabaguliwa, wanawekwa pembeni na kunyimwa fursa za kushiriki kikamilifu katika siasa, uchumi na maendeleo ya jamaa na jamii. Hakika kuwabagua na kuwanyanyasa wanawake ni hasara kubwa kwa taifa kwa kila hali!
Mwisho, tunasisitiza, ingawa kuna mambo na matatizo halisi ambayo yanawahusu wanawake kama wanawake na ambayo yanavuka misingi ya kitabaka, la msingi ni kuwa wanawake na wanaume wote wanaishi katika jamii. Na jamii ya Kenya na Afrika imegawanyika kitabaka, tabaka la wengi mafukara na wachache matajiri. Sawa na mwanamume, mwanamke wa kutoka tabaka la mafukara hawezi kuwa sawa na mwanamke kutoka tabaka la matajiri. Tukizingatia jamii ya Kenya yenye mfumo wa ubepari, wanawake wa tabaka la mabepari wanaungana na wanaume wao kuwanyonya na kuwanyanyasa wanawake na wanaume wa tabaka la wafanyikazi na makabwela. Kwani hapawezi kuwa na usawa kati ya matajiri na mafukara, wanyonyaji na wanyonywaji.
Kwa sababu hii, CPK tunaamini kuwa harakati za kitabaka ndiyo msingi wa harakati zingine zote. Bila usawa wa kitabaka hapawezi kuwepo usawa kamilifu wa kijinsia wala ukombozi halisi wa wanawake. Basi mapambano ya ukombozi wa wanawake lazima wakati wote yachukue mwelekeo wa kupigania usawa wa kijinsia na kitabaka sambamba na sawia. Usoshalisti ndiyo barabara sahihi zaidi ya kuelekea katika uhuru na ukombozi wa wanawake na ya kuleta usawa wa kijinsia Kenya na ulimwenguni.
Yadumu mapambano ya ukombozi wa wanawake!
Zidumu haraka za kuleta usawa wa kijinsia!
Zidumu harakati za kikomunisti!
Idumu CPK!
Mwandawiro Mghanga, Mwenyekiti wa CPK