MUKAMI KIMATHI
Alice Mukami
Alice Mukami Kimaathi
Mzalendo Alice Kimaathi
Askari hodari wa Mau Mau
Mukami gorila mashuhuri mijini na vijijini na msituni
Mukami kiongozi wa kikosi kabambe cha wanawake
Mukami na wanawake, wanawake wazalendo wa Mau Mau
Mbiu ya mgambo ilipolia kutangaza vita vya uhuru na mashamba
Vita vya kupambana dhidi ya wakoloni na mahomugadi wao
Mukami hakusitasita aliamua kimoja
Akafuatana na mumewe Kimaathi kwa hiari yake mwenyewe
Akawa sehemu ya maelfu ya wanajeshi wanawake wa Mau Mau
Waliyokuwa sababu ya ufanisi mkuu wa Mau Mau
Mukami alitambua jukumu lake
Kama Mkenya na kama binadamu
Kweli Mukami ni jazanda la ushujaa wa wananchi
Siku ya kuwapamba mashujaa wa uhuru wa Kenya itakapofika
Tutampamba Mukami kwa dhahabu na almasi
Anaishi hadi wa leo Mukami anaishi kwa uzalendo
Anaishi Njabini Nyandarwa Mukami Kimaathi
Serikali ya mahomugadi wa jana na leo inayotutawala
Inaendelea kumnyanyasa mama yetu mpendwa
Inakataa kumuonyesha Mukami kaburi la mumewe Kimaathi
Maadui wakubwa wa uhuru na ukombozi wa taifa letu
Wanaovuruga na kuparaganya historia yetu ya mapambano
Wanaendelea kukana Mau Mau na kina Alice Mukami
Wanaendelea kuwashindilia katika kasumba ya dini
Bali kina Mukami
Hawana haja ya kutambuliwa na wasaliti wa Mau Mau
Wanafahamu
Ingawa juhudi zao ziliung’oa ukolonimkongwe
Mapambano bado yanaendelea
Kwani ukoloni-mamboleo ungalipo
Mukami, bado kina Mukami wanahitajika
Na watahitajika hadi uhuru kamili
Na sisi leo
Lazima tupambane kwa vyovyote vile
Tujikaze kisabuni
Mateso na majaribu tilatila
Tunayaona
Na tutaendelea kuyaona
Mwandawiro Mghanga
Jela Kuu ya Kibos
Juni 4 1988